
Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) inakabiliwa na ongezeko kubwa la maambukizi ya ugonjwa wa Ebola, huku idadi ya wagonjwa ikivuka 6,000 na vifo kufikia karibu 3,000.
Kwa mujibu wa takwimu zilizotolewa na mamlaka za afya nchini humo, hadi Agosti 31, 2026, jumla ya wagonjwa 6,041 walikuwa wamethibitishwa kuwa na Ebola, huku watu 2,911 wakiripotiwa kufariki dunia.
Hali hiyo imeufanya mlipuko huo kuwa miongoni mwa milipuko mikubwa na yenye madhara zaidi kuwahi kutokea nchini DRC.
Shirika la Afya Duniani (WHO) lilisema katika taarifa yake ya Agosti 28 kuwa Ebola imeenea katika maeneo 60 ya afya yaliyopo ndani ya majimbo sita nchini humo.
Kwa mujibu wa WHO, kiwango cha vifo miongoni mwa watu waliothibitishwa kuambukizwa ugonjwa huo kimezidi asilimia 48, hali inayozidisha wasiwasi kwa mamlaka za afya na jamii zilizo katika maeneo yaliyoathirika.
Mlipuko huo unahusishwa na aina ya Bundibugyo ya virusi vya Ebola, huku changamoto kubwa ikiendelea kuwa upatikanaji wa chanjo au tiba maalumu iliyoidhinishwa dhidi ya aina hiyo.
Juhudi za kudhibiti ugonjwa huo pia zimekumbwa na vikwazo kutokana na hali ya vita na ukosefu wa usalama katika baadhi ya maeneo, pamoja na kuhama kwa wananchi na ugumu wa kuwafikia baadhi ya jamii.
Hofu imeongezeka zaidi kutokana na kufunguliwa kwa shule katika baadhi ya maeneo yaliyoathirika, huku wazazi na walimu wakihofia mikusanyiko ya wanafunzi inaweza kuongeza hatari ya maambukizi.
Wataalamu wa afya wameendelea kutoa wito wa kuchukuliwa kwa hatua za haraka na kuimarishwa kwa juhudi za kukabiliana na mlipuko huo, ili kuzuia Ebola kusambaa zaidi ndani ya DRC na hatimaye kuvuka mipaka kwenda nchi jirani.
Stori na Na Nasra | GPL