
Michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika (CAF Champions League) inatarajiwa kuanza rasmi Septemba 4, 2026, huku Tanzania ikiendelea kuwakilishwa na vigogo wake, Simba SC na Young Africans SC.
Simba na Yanga zitaingia kwenye michuano hiyo zikiwa na kumbukumbu ya kutofanya vizuri katika msimu uliopita, ambapo timu zote mbili ziliishia katika hatua ya makundi.
Kwa msimu huu, kila timu inalenga kufanya vizuri zaidi na kusonga mbele katika hatua za juu za mashindano hayo yanayoandaliwa na Shirikisho la Soka Afrika (CAF).
YANGA KUANZA SEPTEMBA 5
Young Africans SC inatarajiwa kuanza safari yake ya Champions League Septemba 5, 2026, kwa kukutana na Gaborone United ya Botswana.
Mchezo huo umepangwa kuchezwa majira ya saa 12 jioni, huku Yanga ikitarajiwa kuingia uwanjani ikiwa na lengo la kupata matokeo mazuri katika mchezo huo.
Gaborone United pia ina historia ya kuwa na uhusiano na soka la Tanzania, kwani timu hiyo iliwahi kunolewa na Dimitry Pantev, ambaye amewahi kuwa kocha wa Simba SC.
SIMBA KUKABILIA MIGHTY WANDERERS
Kwa upande wa Simba SC, timu hiyo inatarajiwa kushuka dimbani Septemba 6, 2026, dhidi ya Mighty Wanderers ya Malawi.
Mchezo huo umepangwa kuanza majira ya saa 9 alasiri.
Mighty Wanderers inaingia kwenye mchezo huo ikiwa imetoka katika kipindi cha mabadiliko baada ya kumtimua kocha wake kufuatia kipigo katika mchezo wa fainali ya ligi ya ndani nchini Malawi.
SIMBA NA YANGA ZATAKIWA KUWA MAKINI
Simba na Yanga zitaingia kwenye michuano hiyo zikiwa na kumbukumbu kwamba katika misimu iliyopita timu kubwa za Tanzania zimewahi kuondolewa na klabu ambazo hazikuwa na majina makubwa katika soka la Afrika.
Hali hiyo inafanya timu hizo mbili kuhitajika kuwa makini, hasa katika michezo ya ugenini, kwani hatua za awali za mashindano ya CAF mara nyingi zimekuwa na matokeo ya kushangaza.
Kwa Simba na Yanga, lengo kubwa msimu huu ni kuvuka hatua za awali na kuhakikisha zinaiwakilisha Tanzania kwa mafanikio zaidi katika michuano ya juu ya klabu barani Afrika.
Stori na Clever Alphonce | GPL