×

ALAF Yaongoza Kipengele Cha Chuma Katika Tuzo za PMAYA

Kampuni ya ALAF Limited imeibuka mshindi wa kwanza katika kipengele cha Chuma na Bidhaa za Chuma katika Tuzo za Rais za Mzalishaji Bora wa Mwaka (PMAYA), toleo la 19.

Ushindi huo umeifanya ALAF kutwaa tuzo hiyo kwa mara ya 17 mfululizo tangu kuanza kushiriki katika tuzo hizo zinazoratibiwa na Shirikisho la Viwanda Tanzania (CTI).

Tuzo hiyo imekabidhiwa na Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Deogratias Ndejembi, katika hafla ya utoaji wa Tuzo za PMAYA.

Akizungumza baada ya ushindi huo, Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano na Uhusiano wa ALAF, Hawa Bayumi, amesema tuzo hiyo ni ishara ya dhamira ya kampuni hiyo katika uzalishaji wenye viwango vya kimataifa, ubunifu na mchango wake katika kukuza sekta ya viwanda nchini.


“Tuzo hii inadhihirisha uwajibikaji wetu katika kuzalisha katika viwango bora duniani, kuwa mstari wa mbele katika uvumbuzi na kuwa sehemu ya ukuzaji wa viwanda Tanzania,” alisema Bayumi.

Bayumi ametoa shukrani kwa CTI, timu nzima ya ALAF pamoja na wateja wanaoendelea kushirikiana na kampuni hiyo katika kujenga na kuendeleza sekta ya ujenzi nchini.
“Asanteni kwa kutuunga mkono na imani yenu kwetu. Pamoja tutaendelea kujenga viwanda imara, jamii imara na Tanzania imara zaidi,” aliongeza.

Ushindi huo unaendelea kuiweka ALAF katika nafasi ya juu miongoni mwa wazalishaji wa bidhaa za chuma nchini, huku kampuni hiyo ikisisitiza dhamira yake ya kuendelea kuwekeza katika ubora, ubunifu na uzalishaji wa bidhaa zinazokidhi viwango vya kimataifa.

Leave a Comment