
Jeshi la Polisi Mkoa wa Mwanza linamshikilia Sabatho Malima Emmanuel, mwenye umri wa miaka 32, mkazi wa Buswelu, Wilaya ya Ilemela, ambaye ni dereva wa basi la Kampuni ya Obadia lenye namba za usajili T 870 DVW, aina ya Yutong.
Dereva huyo anakabiliwa na tuhuma za kuendesha gari kwa uzembe na kuhatarisha maisha ya abiria pamoja na watumiaji wengine wa barabara, baada ya kudaiwa kuwa alikuwa akichati kwa simu huku akiendesha gari.
Kwa mujibu wa taarifa ya Jeshi la Polisi Mkoa wa Mwanza, tukio hilo lilitokea Septemba 5, 2026, majira ya saa 6:40 mchana, katika eneo la Isangijo, Wilaya ya Magu, barabara ya Mwanza–Musoma.
Taarifa hiyo inaeleza kuwa dereva huyo alikuwa akiendesha basi hilo akitokea Nyamongo kuelekea Mwanza, huku akichati kwa simu kuanzia eneo la Lamadi, mkoani Simiyu.
Aidha, dereva huyo anadaiwa kutoa lugha chafu kwa watumiaji wengine wa barabara, kitendo ambacho Jeshi la Polisi limesema ni kinyume cha sheria, kanuni na taratibu za usalama barabarani na usafirishaji.
Polisi imesema kitendo hicho kilihatarisha maisha ya abiria waliokuwa ndani ya basi pamoja na watumiaji wengine wa barabara.