×

Watuhumiwa 199 Wakamatwa Kwa Makosa Mbalimbali Rufiji

Jeshi la Polisi Mkoa wa Kipolisi Rufiji limekamata jumla ya watuhumiwa 199 kwa makosa mbalimbali katika operesheni na misako iliyofanyika kuanzia Agosti 1 hadi 31, 2026.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kipolisi Rufiji, watuhumiwa hao walikamatwa kwa makosa yakiwemo unyang’anyi, wizi, uvunjaji, kupatikana na nyara za Serikali, mali zinazodhaniwa kuwa za wizi, dawa za kulevya na pombe ya moshi (gongo).

Katika operesheni hiyo, Polisi imekamata pikipiki 24 za aina mbalimbali, baadhi zikiwa hazina namba za usajili na zikidaiwa kuwa mali ya wizi. Watu waliokutwa nazo walishindwa kutoa uthibitisho wa umiliki, huku uchunguzi ukiendelea kubaini wamiliki halali.

Aidha, Polisi imewakamata watuhumiwa saba kwa makosa ya uvunjaji, ambapo walikutwa na mali zinazodhaniwa kuwa za wizi pamoja na vifaa vya kuvunjia. Kesi zao zinaendelea katika hatua mbalimbali za kisheria.

Katika mapambano dhidi ya dawa za kulevya, jumla ya kilo 22 na gramu 405 za bangi zilikamatwa pamoja na watuhumiwa 66. Polisi pia ilikamata lita 63 za pombe ya moshi (gongo) na kuwakamata watuhumiwa 11, akiwemo Fatuma Paulo Madebe (40), mkazi wa Mangwi, Wilaya ya Kibiti, aliyekutwa na mtambo wa kutengeneza gongo.

Kwa upande wa kesi zilizofikishwa mahakamani, Polisi Rufiji imesema watuhumiwa 19 wenye makosa mbalimbali, yakiwemo uvunjaji, wizi, ubakaji na kujeruhi, wamehukumiwa na kupewa adhabu mbalimbali, ikiwemo vifungo gerezani.

Katika kesi ya ukatili wa kijinsia, Maneno John Mboko (49), mkazi wa Tambani, Wilaya ya Mkuranga, amehukumiwa kifungo cha miaka 30 jela kwa kumbaka mwanafunzi wa darasa la sita mwenye umri wa miaka 12. Mahakama pia imemuamuru kulipa fidia ya Sh milioni 3 kwa mhanga.

Jeshi la Polisi pia limekamata madereva wanne kwa makosa ya usalama barabarani kupitia mfumo wa ufuatiliaji wa magari (VTS), huku baadhi wakifutiwa madaraja ya leseni na wengine kufikishwa mahakamani.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kipolisi Rufiji amewataka wananchi kuendelea kushirikiana na Jeshi la Polisi katika kufichua uhalifu na wahalifu, huku akisisitiza kuwa operesheni za kupambana na uhalifu zinaendelea.

Leave a Comment