×

Infantino Athibitisha Kugombea tena Urais wa FIFA Mwakani

Rais wa Shirikisho la Kimataifa la Soka (FIFA), Gianni Infantino, amethibitisha kuwa atagombea tena nafasi ya urais wa FIFA katika uchaguzi utakaofanyika Machi 2027, licha ya kukabiliwa na upinzani na shinikizo kutoka baadhi ya vyama vya soka duniani.

 

FIFA imethibitisha leo, Septemba 7, 2026, kwamba Infantino bado ana mpango wa kugombea muhula mwingine.

 

FIFA imesema kuwa hakuna kilichobadilika tangu Infantino alipotangaza mwezi Aprili kwamba angewania tena nafasi hiyo.

 

Infantino, mwenye umri wa miaka 56, amekuwa rais wa FIFA tangu mwaka 2016 na amewahi kuchaguliwa tena mwaka 2019 na 2023. Akishinda uchaguzi wa mwaka 2027, ataendelea kuiongoza FIFA hadi mwaka 2031 uamuzi wake wa kugombea tena unakuja wakati FIFA ikikabiliwa na mgawanyiko kuhusu uongozi wake.

 

Infantino amekosolewa baada ya mpango wa kuhusisha wawekezaji binafsi katika mashindano ya FIFA, ikiwemo Kombe la Dunia, kukataliwa na hatimaye kuachwa mpango huo uliibua upinzani kutoka kwa baadhi ya mashirikisho makubwa ya soka.

 

Miongoni mwa mashirikisho yaliyomkosoa Infantino ni UEFA, AFC na CONCACAF. Hata hivyo, bado anaungwa mkono na baadhi ya vyama vya soka, hususan barani Afrika kupitia CAF na Amerika Kusini kupitia CONMEBOL.

 

Kwa sasa, Infantino ndiye mgombea pekee aliyethibitishwa rasmi kwa uchaguzi huo, ingawa Victor Montagliani, rais wa CONCACAF, ametajwa kama mmoja wa viongozi wanaoweza kumpinga.

Wagombea wengine wana hadi Novemba 18, 2026 kuwasilisha nia zao,uchaguzi huo unatarajiwa kufanyika Machi 2027 mjini Rabat, Morocco, katika kongamano la FIFA.

 

Matokeo yake yanaweza kuwa na umuhimu mkubwa kwa mustakabali wa uongozi wa soka duniani kutokana na mgawanyiko uliopo ndani ya shirikisho hilo.

 

Kwa sasa, Infantino anaendelea na majukumu yake kama rais wa FIFA huku akitarajiwa kukabiliana na changamoto kubwa zaidi za kisiasa katika safari yake ya kutafuta muhula mwingine wa uongozi.

Na Ashura karimu

Leave a Comment