Jeshi la Polisi Mkoa wa Dodoma limekamata jumla ya watuhumiwa 418 kwa makosa mbalimbali katika kipindi cha kuanzia Agosti 12 hadi Septemba 7, 2026, ikiwa ni sehemu ya misako na operesheni za kukabiliana na uhalifu mkoani humo.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Jeshi la Polisi Mkoa wa Dodoma, kati ya watuhumiwa hao, 118 wamekamatwa wakiwa na vitu mbalimbali vinavyodhaniwa kuwa vya uhalifu, ikiwemo mirungi kilo 46 na gramu 805, bangi kilo 3, mafuta ya dizeli dumu 39, box 24 za marumaru (tiles), debe 15 za mpunga, kuku 127, pombe ya moshi lita 5, vipande 30 vya magamba ya kakakuona, pamoja na vifaa mbalimbali vya elektroniki.
Vitu vingine vilivyokamatwa ni majiko manne ya gesi, feni tano, mashine moja ya aluminium, betri nne za gari zenye thamani ya Sh1.8 milioni, sim tank mbili zenye ujazo wa lita 5,000, simu ndogo 26, televisheni tano, laptop moja aina ya Dell, kompyuta mbili aina ya HP, smartphone mbili, redio mbili, power bank moja, blender moja, friji moja, mashine mbili za kunyolea, saa mbili za mkononi na pikipiki 45.
Aidha, Polisi mkoani Dodoma imewashikilia watuhumiwa 16 kwa kesi ya kuharibu miundombinu ya barabara ya mzunuko Ring Road, watuhumiwa saba kwa kuharibu mazingira, mmoja kwa kubaka, wanne kwa mauaji, wanne kwa ramli chonganishi, wawili kwa ukatili dhidi ya mtoto, wawili kwa wizi wa mifugo, huku watuhumiwa 41 wakikabiliwa na kesi za uvunjaji na wengine 211 kwa makosa mbalimbali.
Katika hatua nyingine, kwa upande wa kikosi cha Usalama Barabarani, Jeshi la Polisi limeendelea kutoa elimu kwa watumiaji wa barabara, wakiwemo mashuleni, vijiji vya bodaboda, stendi za mabasi na maeneo mengine.
Hatua hizo zimeelezwa kuwa sehemu ya jitihada za kukabiliana na makosa ya barabarani. Katika kipindi hicho, madereva 15,018 wamekamatwa kwa makosa mbalimbali, ambapo madereva watatu wamefungiwa leseni kwa muda wa miezi mitatu na mmoja kwa miaka mitano kwa makosa ya kuendesha kwa uzembe na kusababisha ajali, kuzidisha abiria na mwendo kasi, huku madereva 10 wakifikishwa mahakamani.

