
Kaliua, Tabora – Septemba 8, 2026. Kampuni ya Mawasiliano ya Yas Tanzania imekabidhi vifaa vya kujifungulia pamoja na vifaa tiba katika Hospitali ya Wilaya ya Kaliua, mkoani Tabora, ikiwa ni sehemu ya mwendelezo wa Kampeni ya Tumaini inayolenga kuchangia kuboresha huduma za afya ya mama na mtoto.
Msaada huo unatarajiwa kupunguza gharama kwa wajawazito wanaofika kujifungua katika hospitali hiyo, hususan wale kutoka familia zenye kipato cha chini, huku ukisaidia hospitali kukabiliana na mahitaji ya vifaa vinavyotumika katika huduma za uzazi.
Miongoni mwa vifaa vilivyokabidhiwa ni maternity kits, vitanda vya uchunguzi kwa wajawazito, kiti mwendo, mashuka, delivery trays pamoja na khanga.

Akizungumza wakati wa makabidhiano hayo, Mkuu wa Yas – Kanda ya Tanganyika Kati, Kamara Kalembo, alisema msaada huo ni sehemu ya mwendelezo wa Kampeni ya Tumaini iliyoanzishwa na wafanyakazi wa Yas kwa lengo la kugusa maisha ya jamii wanayoihudumia.
“Tunajivunia kuwa Mtandao wa Viwango, lakini tunaamini viwango havipaswi kuishia kwenye huduma za mawasiliano pekee. Vinapaswa pia kuonekana katika namna tunavyowajibika kwa jamii,” alisema Kalembo.
Kwa upande wake, Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Wilaya ya Kaliua, Dkt. Dismas Bulunja, alisema hospitali hiyo inakabiliwa na mahitaji makubwa ya huduma za uzazi, akibainisha kuwa zaidi ya akina mama 2,650 wamejifungua katika hospitali hiyo kati ya Januari na Septemba 2026.

Alisema msaada huo utasaidia kupunguza baadhi ya changamoto zinazohusiana na upatikanaji wa vifaa na hivyo kuchangia kuboresha huduma zinazotolewa kwa wajawazito na kina mama wanaojifungua.
Baadhi ya wajawazito waliopokea msaada huo, Tegemea Awadhi, Amrat Dimanga na Asha Haruna, wakazi wa Kaliua, wameeleza kuwa vifaa hivyo vimewasaidia kupunguza gharama za maandalizi ya kujifungua, hasa kwa familia zenye kipato cha chini.
Hospitali ya Wilaya ya Kaliua imekuwa kituo cha tatu kunufaika na Kampeni ya Tumaini, huku Yas Tanzania ikieleza kuwa kampeni hiyo itaendelea kufikishwa katika maeneo mengine nchini kwa lengo la kuchangia upatikanaji wa mazingira bora ya huduma kwa mama na mtoto.