
DAR ES SALAAM, TANZANIA — Wasanii na watayarishaji wa muziki nchini, Aika na Nahreel, wametangaza rasmi ujio wa album yao mpya inayokwenda kwa jina ‘STEPPA’, inayotarajiwa kuachiwa rasmi Septemba 18, 2026.
Kuelekea kutolewa kwa album hiyo, wawili hao tayari wameachia wimbo wa utangulizi uitwao ‘Weird’, ambao umeanza kuvutia hisia za mashabiki na wapenzi wa muziki wanaosubiri kwa hamu kazi yao mpya.
Aika na Nahreel, wanaofahamika zaidi kama Navy Kenzo, walianza safari yao ya kimuziki mwaka 2013 baada ya kukutana nchini India wakati wa masomo yao. Baadaye waliungana katika kundi la Pah One kabla ya kuanzisha Navy Kenzo.

Tangu kuanzishwa kwao, Navy Kenzo wamejijengea nafasi katika muziki wa Afrika Mashariki kupitia mchanganyiko wa Afro-pop, Dancehall na Bongo Fleva, huku wakitoa kazi mbalimbali zilizowapa umaarufu ndani na nje ya Tanzania.
Miongoni mwa kazi zao zilizowahi kufanya vizuri ni pamoja na ‘AIM (Above Inna Minute)’, ‘Story of the African Mob’ na ‘Most People Want This’.
Mbali na muziki, Aika na Nahreel pia ni wanandoa na wazazi wa watoto wawili, jambo ambalo limeufanya ushirikiano wao kuwa wa kipekee kwa kuwa wanaendeleza safari yao ya kimuziki sambamba na maisha ya familia.