
Jeshi la Polisi Mkoa wa Dar es Salaam linamshikilia mtu mmoja, Conrad Agonza Kayoza, mwenye umri wa miaka 35, mkazi wa Lugalo na Mloganzila, Dar es Salaam, kwa tuhuma za kumshambulia askari wa usalama barabarani.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Kamanda Kanda Maalum ya Polisi Dar es Salaam, tukio hilo limetokea Septemba 8, 2026 majira ya saa 1:30 asubuhi eneo la Lugalo, Kinondoni, kwenye barabara ya Bagamoyo.
Taarifa hiyo imeeleza kuwa askari mwenye namba F.8886 SGT Andrew, wa Kikosi cha Usalama Barabarani Kinondoni, akiwa kazini na akitekeleza majukumu yake, alishambuliwa kwa ngumi na mateke na mtuhumiwa huyo.

Inadaiwa kuwa kabla ya tukio hilo, askari huyo alikuwa kazini na alizuia kisheria magari yaliyokuwa yakipita pembezoni mwa barabara katika eneo la “Service Road” nje ya utaratibu uliokuwepo, ikiwemo gari la mtuhumiwa aina ya Toyota Runx lenye namba za usajili T 455 EER.
Kwa mujibu wa Polisi, mtuhumiwa alishuka kwenye gari na kuanza kumshambulia askari kabla ya yeye mwenyewe kushambuliwa na wananchi waliokuwa wamechukizwa na kitendo hicho.
Conrad Agonza Kayoza alipelekwa hospitalini kwa matibabu baada ya kujeruhiwa na amepewa nafuu. Polisi imeeleza kuwa atahojiwa kwa kina ili hatua za kisheria zichukuliwe na mamlaka husika.
Polisi Dar es Salaam imetoa tahadhari kwa wananchi, ikisisitiza kuwa haitavumilia wala kusita kuchukua hatua kali za kisheria dhidi ya mtu yeyote au kundi litakalomshambulia polisi wakati wanatekeleza majukumu yao ya kisheria.
