
Kampuni ya Apple imezindua rasmi iPhone 18 Pro na iPhone 18 Pro Max, ikiwa ni miongoni mwa bidhaa mpya zilizotangazwa katika tukio lake la kila mwaka lililofanyika usiku wa kuamkia leo, Septemba 10, 2026.
Uzinduzi huo umeleta maboresho makubwa katika maeneo ya kamera, utendaji wa simu, matumizi ya akili bandia (AI) na maisha ya betri, huku Apple ikisisitiza kuwa iPhone 18 Pro ndiyo simu yake yenye mfumo wa kamera wa kitaalamu zaidi kuwahi kutengenezwa.
KAMERA YA 48MP YAPEWA UWEZO MPYA
Miongoni mwa maboresho makubwa ni kamera kuu ya 48MP Fusion Main ambayo sasa ina mfumo wa variable aperture, unaomwezesha mtumiaji kudhibiti zaidi kiwango cha mwanga kinachoingia kwenye kamera na kina cha picha.
Apple pia imeongeza Pro Controls ndani ya programu ya kamera, hivyo watumiaji wanaweza kufanya marekebisho ya kitaalamu zaidi wakati wa kupiga picha na kurekodi video. Mfumo huo umeongezewa uwezo wa kupiga picha katika mazingira yenye mwanga mdogo.

Kwa mujibu wa taarifa za Apple, mfumo wa kamera unajumuisha kamera kuu ya 48MP, 48MP Ultra Wide na 48MP Telephoto, huku simu ikiwa na uwezo wa kurekodi video za 4K Dolby Vision hadi fremu 120 kwa sekunde katika baadhi ya mipangilio.
A20 PRO NA AI
iPhone 18 Pro na Pro Max zimepewa A20 Pro, chip mpya inayolenga kuongeza kasi ya utendaji, uwezo wa kushughulikia kazi za AI na ufanisi wa matumizi ya nishati.
Apple pia imeunganisha simu hizo na kizazi kipya cha Apple Intelligence pamoja na Siri AI, huku kampuni ikisisitiza zaidi matumizi ya AI yenye kuzingatia faragha ya mtumiaji.
Aidha, simu hizo zinakuja na next-generation vapor chamber kwa ajili ya kusaidia kudhibiti joto wakati simu inatumika katika kazi nzito kwa muda mrefu.

BETRI YABORESHWA
Apple imefanya maboresho makubwa kwenye uwezo wa betri, ambapo iPhone 18 Pro Max inaweza kufikisha hadi saa 45 za uchezaji wa video, kiwango ambacho Apple inakitaja kuwa ni ongezeko kubwa zaidi la maisha ya betri kuwahi kufanyika kwenye iPhone.
iPhone 18 Pro yenyewe inaweza kufikisha hadi saa 36 za uchezaji wa video, huku zote zikiwa na teknolojia ya kuchaji kwa kasi zaidi.
MUUNDO NA RANGI MPYA
iPhone 18 Pro na Pro Max zinakuja katika rangi nne ambazo ni Black, Silver, Glacier na Burgundy, huku zikiwa na muundo wa aluminium unibody na Ceramic Shield 2 mbele pamoja na Ceramic Shield nyuma.
iPhone 18 Pro ina skrini ya inchi 6.3, wakati Pro Max ikiwa na skrini ya inchi 6.9, zote zikiwa na Super Retina XDR OLED na ProMotion yenye hadi 120Hz.
STORAGE YAFIKIA 2TB
Katika eneo la uhifadhi, Apple imeongeza chaguo la hadi 2TB kwa iPhone 18 Pro na iPhone 18 Pro Max, hatua inayolenga zaidi watumiaji wanaohifadhi kiasi kikubwa cha picha, video na mafaili.
Simu hizo zinapatikana katika viwango vinne vya uhifadhi: 256GB, 512GB, 1TB na 2TB. Hii inampa mtumiaji nafasi kubwa zaidi ya kuhifadhi maudhui bila kutegemea mara kwa mara huduma za uhifadhi wa mtandaoni.
Kwa watengeneza maudhui, wapiga picha na wapiga video, uwezo wa 2TB ni muhimu zaidi kutokana na ukubwa wa mafaili ya video za ubora wa juu. iPhone 18 Pro ina uwezo wa kurekodi video za 4K Dolby Vision hadi 120fps, pamoja na ProRes na ProRes RAW, hivyo nafasi kubwa ya uhifadhi inaweza kuwa na manufaa kwa kazi za kitaalamu za video.
Kwa hiyo, iPhone 18 Pro na iPhone 18 Pro Max hazijaongezewa tu nguvu ya kamera na utendaji, bali pia zimepewa nafasi kubwa zaidi ya kuhifadhi inayofikia 2TB, ikiwa ni chaguo la juu zaidi katika mfululizo huo.
BEI NA UPATIKANAJI
Kwa Marekani, iPhone 18 Pro inaanzia dola 1,199 sawa na TSh milioni 3, wakati iPhone 18 Pro Max inaanzia dola 1,299 sawa na TSh milioni 3.31. Hii ni ongezeko la dola 100 kwa kila toleo ikilinganishwa na bei za kuanzia za kizazi kilichotangulia, huku Reuters ikiripoti kuwa kupanda kwa gharama za chips za kumbukumbu ni miongoni mwa sababu zilizochangia ongezeko hilo.
Apple imesema oda za awali (pre-orders) zitaanza Septemba 12, huku simu hizo zikianza kupatikana rasmi madukani na kwa wateja kuanzia Septemba 18, 2026.
Uzinduzi wa iPhone 18 Pro umefanyika sambamba na tangazo la iPhone Duo, simu ya kwanza ya Apple yenye skrini inayokunjika, pamoja na bidhaa mpya za Apple Watch na AirPods.