×

Kabla Ya Gaborone, Nondo Afunguka Kiwango Chake Msimu Huu

Nahodha wa Yanga SC, Bakari Nondo, amesema sababu kubwa ya kurejea kwenye kiwango bora ni maandalizi mazuri pamoja na ushirikiano anaoupata kutoka kwa wachezaji wenzake.

Nondo alianza katika kikosi cha kwanza cha Yanga SC kwenye mchezo wa hatua ya awali ya Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Gaborone United, uliomalizika kwa sare ya bao 1-1. Bao la Yanga SC lilifungwa na Seleman Mwalimu dakika ya 90.

Akizungumza kuhusu kurejea kwake kwenye kiwango bora, Nondo amesema kuanza msimu vizuri ni jambo la kumshukuru Mungu, huku akitaja maandalizi kuwa sehemu muhimu ya mafanikio yake.
“Kuanza msimu vizuri ni jambo la kushukuru. Msimu wa mwaka jana sikuwa na kiwango bora, lakini msimu huu namshukuru Mwenyezi Mungu kwa sababu ninapata nafasi. Kujiandaa vizuri ni kitu cha muhimu kuhusu kuwa bora kwenye mchezo,” amesema Nondo.

Nondo pia amezungumzia mchezo wa kwanza dhidi ya Gaborone United uliochezwa ugenini, akieleza kuwa alilazimika kusogea mbele kutokana na wapinzani kucheza muda mwingi wakiwa nyuma.
“Kuhusu mchezo wetu uliopita dhidi ya Gaborone United ugenini, ilikuwa ni lazima nipande juu kwa kuwa wale wenzetu muda mwingi walikuwa wanacheza wakiwa nyuma, hivyo nilikuwa ninapata muda wa kusogea mbele,” amesema.

Yanga SC inatarajiwa kukutana tena na Gaborone United Septemba 12, 2026, katika Uwanja wa Azam Complex, kwenye mchezo wa marudiano wa hatua ya awali ya Ligi ya Mabingwa Afrika.

Mshindi wa jumla katika michezo hiyo miwili atasonga mbele kwenda hatua inayofuata ya michuano hiyo.

Stori na Witnes Godfrey | GPL – TUDACO

Leave a Comment