×

Kesi Ya Ugaidi: Mhadhiri Udom Melkisedek Kaijage Aachiwa Huru

Mahakama ya Hakimu Mkazi Dodoma imemwachia huru Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM), Melkisedek Kitunzi Kaijage, baada ya upande wa Jamhuri kueleza kuwa hauna nia ya kuendelea na mashtaka yaliyokuwa yakimkabili.

Kaijage aliachiwa huru Alhamisi, Septemba 10, 2026, mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Denisi Mpelembwa.

Mwendesha Mashtaka Mwandamizi wa Serikali, Jonathan Chuwa, aliiambia mahakama kuwa Jamhuri haikuwa na nia ya kuendelea na mashtaka dhidi ya Kaijage, yaliyohusisha makosa ya ugaidi na uhujumu uchumi. Chuwa aliomba mahakama kumwachia huru, akifafanua kuwa uamuzi huo unahusu mashtaka yaliyokuwa mbele ya mahakama hiyo pekee.

Kaijage alikamatwa Julai 8, 2026, kufuatia tuhuma za kuhusika katika kuhamasisha maandamano yaliyokuwa yamepangwa kufanyika Julai 7. Awali alishikiliwa kwa tuhuma hizo kabla ya mashtaka kubadilishwa na kuwa ya ugaidi na uhujumu uchumi.

Katika mashtaka yaliyowasilishwa mahakamani, Jamhuri ilidai kuwa Julai 3, 2026, akiwa katika maeneo ya UDOM, Kaijage alitishia kuchoma majengo ya umma pamoja na makazi ya polisi kwa lengo la kuwatisha wananchi.

Kesi hiyo iliwasilishwa chini ya vifungu vya Sheria ya Kuzuia Ugaidi pamoja na Sheria ya Udhibiti wa Uhalifu wa Kiuchumi na Kupangwa.

Kaijage alikaa rumande wakati shauri hilo likiendelea katika hatua za awali, huku mahakama ikitarajiwa kuendelea na taratibu za uchunguzi wa awali kabla ya shauri kupelekwa Mahakama Kuu.

Hata hivyo, kabla ya kuachiwa, Mkuu wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai Mkoa wa Dodoma (RCO) aliwasilisha maombi ya kuwekwa chini ya masharti maalumu baada ya kuachiwa.

Mahakama ilikubaliana na baadhi ya masharti hayo. Kaijage ametakiwa kuwa na wadhamini wawili, ambao ni wakazi wa Mkoa wa Dodoma, kila mmoja akisaini dhamana ya maneno ya Sh milioni tano.

Aidha, wadhamini hao wanatakiwa kuwa na barua za utambulisho pamoja na vitambulisho halali. Kaijage pia ametakiwa kuripoti kwa RCO kila Ijumaa ya mwisho wa mwezi saa 2:30 asubuhi kwa kipindi cha mwaka mmoja.

Leave a Comment