
Mshambuliaji wa Simba SC, Ibrahim Doumbia, ni miongoni mwa wachezaji wanaoendelea na mazoezi maalumu kuelekea mchezo wa marudiano wa hatua ya awali ya Ligi ya Mabingwa Afrika (CAF Champions League) dhidi ya Mighty Wanderers ya Malawi.
Mchezo huo unatarajiwa kuchezwa Septemba 13, 2026, katika Uwanja wa Uhuru jijini Dar es Salaam, huku Simba SC ikiwa na faida ya ushindi wa bao 1-0 iliyoupata katika mchezo wa kwanza ugenini.
Bao pekee la Simba SC katika mchezo huo lilifungwa na Anicet Oura dakika ya 65, hivyo Wekundu wa Msimbazi kuhitaji matokeo yatakayowavusha kwenda hatua inayofuata.

Kocha Mkuu wa Simba SC, Steve Barker, anaendelea kuwaandaa wachezaji wake kwa mchezo huo, akiwemo Oura, Doumbia, Clatous Chama, Ellie Mpanzu na Hussen Abel.
Barker amesema mchezo huo hautakuwa rahisi kutokana na Mighty Wanderers kuhitaji ushindi wakiwa ugenini, akisisitiza kuwa Simba bado haijafuzu licha ya kushinda mchezo wa kwanza.
“Wapinzani wetu wanatambua kwamba wamepoteza mchezo wa kwanza, hivyo wanakuja kwenye mchezo wakiwa wanahitaji ushindi. Tunawaheshimu wapinzani kutokana na ubora walionao kwani kazi bado inaendelea.”
Amesema pia kikosi chake kinaendelea kufanyia kazi makosa yaliyojitokeza katika mchezo wa kwanza ili kuhakikisha kinafanya vizuri zaidi katika mchezo wa marudiano.
“Makosa ambayo yamepita tunafanyia kazi ili kuwa bora zaidi. Hauwezi kuwa mchezo rahisi. Matokeo ya mwisho yataamua nani ambaye atafuzu hatua inayofuata. Hata sisi bado hatujafuzu, tunapambana kuhakikisha tunafanikisha malengo yetu.”
Stori na Lunyamadzo Mlyuka