×

Heche Ahojiwa Kuhusu Ripoti Za Uchaguzi Alizozitumia Mahakamani, Akanusha Kupata Division Four

Dar es Salaam, Septemba 14, 2026 — Makamu Mwenyekiti wa Chadema, John Heche, ameendelea kuhojiwa mahakamani katika kesi inayomkabili Mwenyekiti wa chama hicho, Tundu Lissu, huku upande wa serikali ukimhoji kuhusu wasifu wake, mali, madai ya mauaji, utekaji na taarifa za uchaguzi alizozitoa katika ushahidi wake.

Katika sehemu ya maswali kuhusu elimu yake, Heche ameiambia mahakama kuwa ana Shahada ya Elimu na Sanaa (Bachelor of Arts with Education) na kwamba baada ya kumaliza A-Level alisoma diploma ya ualimu kabla ya kuendelea na masomo ya chuo kikuu.

Wakili Nassor Katuga pia alimuuliza kuhusu jina alilotumia katika masomo yake ya msingi hadi sekondari, ambapo Heche alithibitisha kuwa alisoma kwa jina la Wegesa Charles Suguti. Aidha, alikanusha madai kwamba alipata Division Four katika mtihani wa kidato cha nne, akisema alipata Division One ya pointi 11.

Katika maswali kuhusu mali, Heche alikiri kuwa anamiliki magari, huku maelezo ya majadiliano mahakamani yakihusu taarifa za umiliki wa magari zinazohifadhiwa na TRA.

Madai ya mauaji na utekaji

Katika sehemu nyingine ya maswali, Wakili Ignas Mwinuka alimuuliza Heche kuhusu orodha ya watu aliowataja katika madai ya mauaji. Heche alisema hakushuhudia kwa macho yake baadhi ya matukio aliyoyataja, akiwemo mtu aliyemtaja katika tukio la Arumeru na mwingine katika tukio la Ezekiel Wenje.

Heche pia alikiri kuwa hakueleza mahakamani taarifa za kitabibu kuhusu chanzo cha vifo vya watu aliowataja na kwamba hakushiriki katika uchunguzi wa miili yao.

Kuhusu madai ya utekaji na watu kupotea, Heche aliiambia mahakama kuwa hajawahi kushuhudia mtu akitekwa kwa macho yake wala kushuhudia mtu yeyote kati ya aliowataja akipotea.

Ripoti za uchaguzi

Wakili Mwinuka pia alihoji kuhusu ripoti mbalimbali za uchaguzi ambazo Heche alizitaja katika ushahidi wake. Heche alisema ripoti hizo alizipata kupitia vyombo vya habari.

Alithibitisha kuwa ripoti za Thabo Mbeki Foundation, Umoja wa Mataifa, Human Rights Watch, Jumuiya ya Madola, Umoja wa Afrika na waangalizi wa SADC zilikuwa kwa kiasi kikubwa zimeandikwa kwa Kiingereza.

Alipoulizwa kama yeye ndiye aliyefasiri taarifa hizo kutoka Kiingereza kwenda Kiswahili wakati akitoa ushahidi mahakamani, Heche alikubali. Hata hivyo, alisema hakueleza mahakamani kuhusu umahiri wake wa lugha uliomwezesha kufanya tafsiri hizo.

Tukio la Septemba 7, 2017

Katika maswali kuhusu tukio la kushambuliwa kwa Tundu Lissu Septemba 7, 2017, Heche alisema hakuwapo eneo la tukio na kwamba maelezo aliyoyatoa kuhusu shambulio hilo yalitokana na maelezo aliyotoa Lissu mwenyewe.

Heche pia alisema anakumbuka Spika wa Bunge wakati huo kutoa taarifa ya kulaani tukio hilo, huku akisema hakumbuki kama Rais wa wakati huo, John Magufuli, na Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Humphrey Polepole, walitoa taarifa za kulaani au kusikitishwa na tukio hilo.

Usikilizwaji wa kesi unaendelea, huku upande wa serikali ukiendelea kumuuliza Heche kuhusu madai mbalimbali aliyoyatoa katika ushahidi wake wa msingi, ikiwemo masuala ya uchaguzi, mashambulizi, utekaji, mauaji na ripoti za waangalizi wa kimataifa.

Katuga: Kwa maneno rahisi wewe ni mwalimu

Heche: Sahihi

Katuga: Ulienda moja kwa moja

Heche: Nilienda chuo cha ualimu diploma kisha nienda tena digrii

Katuga: Umesoma kwa jina la wegesa chacha suguta

Heche: Sahihi

Katuga: Ulipata four form four (Division 4 kidato cha 4)

Heche: Uongo nilipata 1.11

Katuga: Mbali ya kuwa makamo mwenyekiti

Katuga: Umeiambia mahakama kama una kitu kingine cha kuingiza kipato

Heche: Sikuiambia

Katuga: Umeiamba Mahakama kama unalipa posho au mshahara

Heche: Sikuulizwa

Katuga: Umeiambia

Heche: Sikuiambia

Katuga: Una Malori yanafanya kazi Kenya

Hecha: Sina mimi ni mkulima

Katuga: Una magari manne ya bei mbaya

Heche: Nina magari mawili bei mbaya sijui ni kitu gani

Katuga: Unajua taarifa za umiliki wa magari zinahifadhiwa TRA

Heche: Ndio

Katuga: Hizi kadi ni ngapi

Heche: Tano

Katuga: Zimesajiliwa kwa majina gani

Heche: Majina yangu

Katuga: Mfumo wa TRA unakusoma una vitu vitano

Heche: Ndio

Katuga: Kiutaratibu wa chama zile tone tone kiongozi akipokea michango anafanya nini

Heche: Masuala ya fedha yako chini ya Katibu Mkuu

Katuga: Unafanya nini

Heche: Napokeaje pesa

Katuga: Pesa ulizopokea kwa Nilesh ulifanya nini

Heche: Simjui huyo mtu

Katuga: Uliwaaambia majaji ulisoma taarifa ya TLS

Heche: Ndio

Katuga: Waambie majaji ilikuwa ya lini

Heche: Nilisema ya 2026 sikumbuki tarehe

Katuga: Nimekusikia ukisema taarifa nyinge iliandikwa kwa kingereza

Heche: Ndio

Katuga: Na ya TLS iliandikwa kwa kingereza

Katuga: Ripoti ya TLS

Katuga: Kuna mtu ulimtaja anaitwa Saimon Kanguye

Heche: Ndio

Katuga: Alitekwa lini

Heche: Kati ya mwaka 2017 hapo

Katuga: Una fahamu kama kuna matukio ya kijinai ya watu kuwaua watu kwa visasi

Heche: Sifahamu

Katuga: Hii taarifa ya TLS ya mwaka 2024 jina la mwisho ni la nani

Heche: Saimon Kanguye

Katuga: Umesema ulipata taarifa ya kutekwa kwakwe kwenye vyombo vya Habari. Chombo gani

Heche: Sikumbuki

Katuga: Uliwahi kuchunguza Kanguye

Heche: Familia yake ilisema ametoweka ametekwa

Wakili Katuga: Unajua au hujui kwamba lengo la kukuuliza maswali haya ni kuifanya mahakama ipime uaminifu wa ushahidi wako?

Heche: Wa uongo au wa ukweli?

Wakili Katuga: Waambie majaji, ni kweli baba yako anaitwa Charles Heche Suguye?

Heche: Ndiyo.

Wakili Katuga: Una elimu gani?

Heche: Shahada ya Elimu na Sanaa (Bachelor of Arts with Education).

Wakili Katuga: Wewe ni mwalimu?

Heche: Ndiyo.

Wakili Katuga: Uliendaje kusoma shahada hiyo?

Heche: Nilimaliza A-Level, nikaenda chuo cha ualimu kusoma diploma, kisha baadaye nikaenda chuo kikuu.

Wakili Katuga: Ni kweli kwamba kuanzia shule ya msingi hadi sekondari ulisoma kwa jina la Wegesa Charles Suguti?

Heche: Ni kweli.

Wakili Katuga: Ni kweli kidato cha nne ulipata Division Four ya alama 27?

Heche: Siyo kweli.

Wakili Katuga: Ulipata Division ngapi?

Heche: Division One.

Wakili Katuga: Ya pointi ngapi?

Heche: Pointi 11.

Wakili Katuga: Mbali na kuwa Makamu Mwenyekiti wa Chadema, umeiambia mahakama kwamba unajiingizia kipato kupitia shughuli gani?

Heche: Sijaiambia.

Madai ya kutekwa na kupotea

Wakili Mwinuka: Wewe binafsi umewahi kushuhudia mtu akitekwa kwa macho yako?

Heche: Kwa macho yangu sijawahi kushuhudia.

Wakili Mwinuka: Umewahi kushuhudia mtu akipotea kati ya hao uliowataja?

Heche: Hapana.

Wakili Mwinuka: Kuhusu Tume ya Chande ya Oktoba 29, msimamo wa Chadema ulikuwa upi?

Heche: Msimamo wetu ulikuwa kwamba tume hiyo haikuaminika kwa sababu iliundwa katika mazingira ya kuficha ukweli kuhusu waliohusika.

Wakili Mwinuka: Kwa msimamo huo, hamkutoa ushirikiano kwa tume hiyo?

Heche: Sahihi.

Wakili Mwinuka: Katika ripoti ulizozitaja kuhusu uchaguzi mkuu wa mwaka jana, ripoti ya Afrika Mashariki ilisema nini?

Heche: Ilisema uchaguzi ulikuwa mzuri, wa haki na haukuwa na tatizo lolote.

Wakili Mwinuka: Kuhusu ripoti nyingine za kikanda na kimataifa, hukueleza ulizipata wapi, ni kweli?

Heche: Nilieleza kwamba nilizipata kupitia vyombo vya habari.

Wakili Mwinuka: Kwa hiyo ulizipata kupitia Google?

Heche: Nilieleza nilikozipata.

Wakili Mwinuka: Ripoti ya Thabo Mbeki Foundation iliandikwa kwa lugha gani?

Heche: Kiingereza.

Wakili Mwinuka: Hii ya UN je?

Heche: Kiingereza, lakini pia waliandika kwa lugha nyingine.

Wakili Mwinuka: Human Rights Watch?

Heche: Kiingereza.

Wakili Mwinuka: Jumuiya ya Madola?

Heche: Kiingereza pia.

Wakili Mwinuka: Taarifa ya AU?

Heche: Kiingereza.

Wakili Mwinuka: Waangalizi wa SADC?

Heche: Kiingereza pia.

Wakili Mwinuka: Utakubaliana kwamba wewe ndiye ulifasili taarifa hizi kutoka Kiingereza kwenda Kiswahili hapa mahakamani?

Heche: Sahihi.

Wakili Mwinuka: Hukueleza umahiri wako wa lugha uliokuwezesha kufanya tafsiri hizo?

Heche: Sikueleza.

Wakili Mwinuka: Unakubaliana kwamba tafsiri inaweza kubadili maana kulingana na umahiri wa mfasiri?

Heche: Sijui.

Wakili Mwinuka: Kuhusu madai ya mauaji, umetaja orodha ya waliouawa. Je, wewe uliwahi kushuhudia kwa macho yako?

Heche: Nilikuwepo Nyamongo siku ya kufunga kampeni…

Wakili Mwinuka: Ni mauaji mangapi uliyashuhudia kwa macho yako?

Heche: Hadi niorodheshe? Ndiyo maana nimeanza kueleza.

Wakili Mwinuka: Ni mauaji mangapi uliyashuhudia kwa macho yako?

Heche: Sijui ni mangapi.

Wakili Mwinuka: Kuhusu mauaji ya Arumeru, ulimtaja nani?

Heche: Msafiri Mbwembwe.

Wakili Mwinuka: Wewe ulikuwepo wakati tukio hilo linatokea?

Heche: Sikuwepo.

Wakili Mwinuka: Kuhusu tukio la Ezekiel Wenje, ulisema nani alipata tukio?

Heche: Nyatega Wenje.

Wakili Mwinuka: Katika hayo mauaji uliyoyaeleza, ulikuwepo eneo la tukio?

Heche: Sikuwepo.

Wakili Mwinuka: Unatambua kwamba chanzo cha kifo kisheria lazima kithibitishwe na taarifa ya kitaalamu?

Heche: Ni sahihi.

Wakili Mwinuka: Kwa mauaji yote uliyoyaeleza hapa mahakamani, umeeleza chanzo cha kifo kwa mujibu wa taarifa za kitabibu?

Heche: Sikueleza taarifa za kitabibu.

Wakili Mwinuka: Umewahi kushiriki kama shahidi katika uchunguzi wa miili ya watu hao?

Heche: Sikushiriki.

Leave a Comment