
Arusha. Binti mwenye umri wa miaka 24, Irene Mallya, mkazi wa Mtaa wa Lemara, Kata ya Lemara jijini Arusha, amefariki dunia baada ya kudaiwa kujeruhiwa wakati akijaribu kuamulia ugomvi kati ya rafiki zake.
Kwa mujibu wa mama mzazi wa marehemu, Mariam Selemani, tukio hilo lilitokea Septemba 14, 2026, majira ya saa 12 asubuhi, baada ya baadhi ya marafiki wa Irene kufika nyumbani na kumtaarifu kuwa binti yake alikuwa amejeruhiwa na kukimbizwa hospitalini.
Mariam amesema taarifa alizopewa kuhusu mazingira ya tukio hilo zilikuwa zikitofautiana, akieleza kuwa awali aliambiwa Irene alikuwa akihusika katika ugomvi huo, kabla ya baadaye kupewa taarifa kwamba alikutwa amelala nje huku akitokwa na damu muda mfupi baada ya kujaribu kuamulia ugomvi.
Kutokana na taarifa hizo zinazotofautiana, familia bado inasubiri uchunguzi wa mamlaka kubaini mazingira halisi yaliyopelekea Irene kujeruhiwa na hatimaye kufariki dunia.
Wakati huo huo, watu wawili waliokuwa karibu na marehemu wanashikiliwa na Jeshi la Polisi kwa ajili ya mahojiano, huku uchunguzi ukiendelea kubaini chanzo cha tukio hilo na iwapo kuna mtu anayehusika na kifo hicho.

The Hub yakanusha kuhusishwa na tukio
Katika hatua nyingine, uongozi wa The Hub Arusha umekanusha taarifa zinazosambaa kwenye mitandao ya kijamii zinazohusisha eneo hilo na tukio la kifo cha Irene Mallya.
Katika taarifa iliyotolewa Septemba 15, 2026, uongozi wa The Hub umesema tukio hilo halikutokea ndani ya The Hub wala ndani ya eneo lao la biashara.
Uongozi huo umesema umesikitishwa na taarifa zisizo sahihi zinazosambazwa na kuhusisha eneo hilo na tukio hilo, huku ukitoa pole kwa familia ya Irene, ndugu, marafiki pamoja na wote walioguswa na msiba huo.
“Tukio hilo halikutokea ndani ya The Hub wala ndani ya eneo letu la biashara,” uongozi huo umesisitiza katika taarifa yake.
The Hub imesema inaendelea kuheshimu uchunguzi unaofanywa na mamlaka husika na iko tayari kutoa ushirikiano pale itakapohitajika.
Aidha, uongozi huo umesisitiza kuwa usalama na ustawi wa wateja pamoja na wafanyakazi ni miongoni mwa vipaumbele vyao.
The Hub imeviomba vyombo vya habari, waendeshaji wa kurasa za mitandao ya kijamii na wananchi kwa ujumla kuhakikisha wanathibitisha taarifa kabla ya kuzichapisha au kuzisambaza, ili kuepusha kuenea kwa taarifa potofu zinazoweza kulihusisha eneo hilo na tukio la kifo cha Irene Mallya.
Uchunguzi wa Jeshi la Polisi unaendelea ili kubaini kwa undani mazingira ya tukio hilo.