×

Heche: Lissu Hakutupa Maelekezo ya Kuzuia Uchaguzi wala Kuhamasisha Uasi

Dar es Salaam. Shahidi John Heche ameiambia mahakama kuwa Tundu Lissu hakuwahi kuwapa maelekezo ya namna ya kuzuia Uchaguzi Mkuu, kuhamasisha uasi au kufanya vitendo vya kuvuruga uchaguzi.

Heche ametoa kauli hiyo wakati akihojiwa na Wakili Katuga, katika sehemu ya mahojiano iliyolenga kuchunguza kauli na misimamo ya viongozi wa CHADEMA kuhusu Uchaguzi Mkuu wa 2025.

Akijibu swali la Katuga kama Lissu aliwaambia njia za kuzuia uchaguzi, Heche alisema: “Hakutuambia.”

Alipoulizwa kama Lissu aliwaambia njia za kuhamasisha uasi, shahidi huyo alijibu tena: “Hakutuambia.”

Aidha, alipoulizwa kama Lissu aliwahi kutaja njia ya kukinukisha, Heche alisema: “Hakusema.”

Hata hivyo, katika mahojiano hayo Heche alikiri kwamba alimsikia mwenyekiti wa chama akisema, “tutazuia uchaguzi.”

Pia alikiri kuwa mwenyekiti alisema “mahakamani hakuendeki” na kwamba polisi wanaingiza kura feki.

“No Reforms, No Election”

Kabla ya kufikia hoja hizo, Katuga alimuuliza Heche kama baada ya Lissu kukamatwa aliendeleza nia ya kuzuia uchaguzi.

Heche hakukubaliana na swali hilo, akisema alichokiendeleza kilikuwa msimamo wa “No Reforms, No Election.”

Alipoulizwa tena kama msimamo huo ulikuwa nia ya kuzuia uchaguzi, Heche alijibu:

“Hicho unachouliza siyo kweli.”

Katuga aliendelea kumkabili kuhusu kauli zinazodaiwa kutolewa kupitia vyombo vya habari kwamba uchaguzi wa 2025 hautafanyika.

Katika maswali hayo, Heche alisema mara kadhaa “sikumbuki”, ikiwemo alipoulizwa kuhusu mahojiano yake na East Africa Radio na kauli zinazodaiwa kutolewa kuhusu kutoshiriki uchaguzi na kutofanyika kwa uchaguzi.

Mahakama yakataa kusikiliza sauti

Wakati Katuga akiomba Heche akumbushwe kwa kutumia rekodi ya sauti ya mahojiano yake ya East Africa Radio, Lissu alipinga hatua hiyo na kurejea kifungu cha 177(1) na (2) cha Sheria ya Ushahidi.

Majaji, kwa mujibu wa mwenendo uliowasilishwa mahakamani, waliamua kwamba Heche akumbushwe bila kusikiliza sauti hiyo.

Baada ya kukumbushwa, Heche bado alisema hakumbuki baadhi ya kauli alizoulizwa.

Ushahidi kuhusu Oktoba 29

Katuga pia alimhoji Heche kuhusu hotuba ya Jaji Chande na matukio ya Oktoba 29.

Heche alisema anakumbuka kwamba katika hotuba hiyo ilielezwa kuwa matukio hayo yalipangwa na kuratibiwa, lakini alisema hakumbuki baadhi ya vipengele vingine alivyoulizwa.

Alikanusha kuwa anakumbuka kama alisema hotuba hiyo ilieleza kwamba fujo za Oktoba 29 zililenga kuzuia uchaguzi.

Aidha, hakukumbuka baadhi ya maelezo kuhusu idadi ya askari waliouawa.

Mkutano wa CHADEMA

Katika sehemu nyingine ya ushahidi, Heche alikiri kwamba alihudhuria mkutano wa CHADEMA ambapo mwenyekiti wa chama taifa alikuwa mzungumzaji mkuu.

Heche alisema naye alizungumza katika mkutano huo kwa muda wa takribani nusu saa, ingawa hakukumbuka kwa usahihi alichokizungumza.

Katuga alitaka kujua kama kulikuwa na hotuba rasmi iliyoandaliwa na mwenyekiti kwa ajili ya mkutano huo. Heche alisema hafahamu.

Pia alisema mikutano ya CHADEMA si yote huhifadhi kumbukumbu.

Hoja inayobaki mbele ya mahakama

Ushahidi wa Heche umeibua tofauti kati ya msimamo wa kisiasa wa “No Reforms, No Election” na madai kwamba kulikuwa na mpango au maelekezo ya moja kwa moja ya kuzuia uchaguzi.

Wakati Heche akikiri kusikia baadhi ya kauli kali kuhusu uchaguzi, amesisitiza kwamba Lissu hakuwahi kuwapa maelekezo ya namna ya kuzuia uchaguzi au kuhamasisha uasi.

Hivyo, mahojiano ya Katuga yanaendelea kulenga kubaini kama kauli na matendo yaliyotajwa mahakamani yanaonyesha msimamo wa kisiasa pekee au yanaweza kuhusishwa na madai ya njama ya kuzuia uchaguzi.

Katuga: Ni kweli au si kweli, baada ya mshtakiwa kukamatwa kwa kesi hii, wewe uliendeleza nia ya kuzuia uchaguzi mkuu, ni kweli au siyo kweli?

Heche: Niliendeleza msimamo wa no Reforms No Election

Katuga: Ni kweli au si kweli wewe uliendeleza nia ya kuzuia uchaguzi

Heche: Hicho unachouliza siyo kweli.

Wakili Katuga: Unakumbuka au hukumbuki kupitia vyombo vya habari uliwahi kutangaza uchaguzi wa 2025 hautofanyika?

Heche: Sikumbuki .

Katuga: Unakumbuka au hukumbuki kwamba ulieleza katika kuzuia uchaguzi mlionana na watu mbali mbali wa dini?

Heche: Sikumbuki

Katuga: Sema kama ulieleza kwamba mliwatembelea viongozi wa dini.Nilieleza waeleze majaji kama kuna ufanano je ushahidi wa kuwatembelea viongozi wa dini na huu uliotoa hapa mahakamani unafanana au haufanani

Heche: Mimi sikumbuki.

Katuga: Unakumbuka au hukumbuki, uliutangazia umma wa watanzania kupitia EA radio kwamba siyo tu chadema hawatashiriki bali uchaguzi hautafanyika.

Heche: Nilishakwenda pale maranyingi, sikumbuki.

Katuga: Upo tayari kukumbushwa?

Heche: Sipo tayari. (Wakili katuga akaomba mahakama imkumbushe Heche kwa ushahidi huo wa sauti akiwa East Africa Radio (EA radio)

Lissu akasimama na kutaka wakili wa serikali asiruhusiwe kufanya anachotaka kufanya yaani kuthibitisha maneno yake kwa njia ya sauti. Huku Lissu akirejea kifungu husika cha 177 (1) na 2 cha sheria ya ushahidi) akisema jambo hilo haliwezekani.

Majaji wakasema kwamba akumbushwe na asikilizishwe sauti hiyo.

Katuga: Waambie majaji hiyo nyara, hicho ukichosikia, je kina ushahidi wowote unaofanana na ushahidi wa msingi ulioutoa?

Heche: Sahihi.

Katuga: Ni kweli hiyo nyaraka inastahili na kwamba mtaonana na watu waliowahi kuwa viongozi?

Heche: Ni sahihi

Katuga: Ni sahihi jana ulisema mlionana na Mzee Warioba?

Heche: Nilisema.

Katuga: Ni kweli au sio kweli kwamba uliwahi kuzungumza na EAradio?

Heche: Sikumbuki.

Katuga: Pamoja na kukumbushwa bado hukumbuki?

Heche: Sijui sikumbuki.

Katuga: Waambie majaji ni wewe ulieeleza kwamba ulisikiliza hotuba ya jaji chande yote.

Heche: Nilieleza jana.

Katuga: Ulieleza kwamba fujo za Oktoba 29 zililenga kuzuia uchaguzi?

Heche: Eneo hilo sikumbuki.

Katuga: Unakumbuka au hukumbuki kwamba hotuba ya jaji chande ilisema fujo zile zilisababishwa na viongozi wa vyama vya siasa waliokuwa na madai mengi ya mabadiliko ya mfumo wa uchaguzi?

Heche: Sikumbuki

Katuga: Unakumbuka ulisema jaji chande alisema askari 16 waliuawa

Heche: Sina kumbukumbu hiyo.

Katuga: Unakumbuka jaji chande kama anasema matukio yale yalipangwa na kuratibiwa?

Heche: Hiyo nakumbuka.

Katuga: Waambie majaji kama unakumbuka ulisema mpo determined kupitia ushindi uliopewa?

Heche: Maneno hayo yapo.

Katuga: Ulisema hakuna makosa ya kuzuia uchaguzi?

Heche: Nilisema

Katuga: Kwa uelewa wako mdogo wa sheria, ni sheria ipi inasema hayakuwa makosa kuzuia uchaguzi?

Heche: Kwa ufahamu wangu.

Wakili Katuga: Waambie majaji, mbali na mwaliko, kama unafahamu au hufahamu kulikuwa na hotuba rasmi aliyoandaliwa mwenyekiti.

Heche: Sifahamu.

Wakili Katuga: Mikutano ya CHADEMA huwa inahifadhi kumbukumbu?

Heche: Siyo yote.

Wakili Katuga: Nani alikuwa mzungumzaji mkuu?

Heche: Mwenyekiti wa Chama Taifa.

Wakili Katuga: Waambie majaji wewe kama wewe ukiongea kwenye huo mkutano?

Heche: Niliongea.

Wakili Katuga: Muda gani?

Heche: Nadhani kama nusu saa, sikumbuki.

Wakili Katuga: Waambie majaji kama umeiambia Mahakama siku hiyo ya mkutano uliongea nini.

Heche: Sikumbuki.

Wakili Katuga: Ulimsikia mwenyekiti akisema tutazuia uchaguzi?

Heche: Ndiyo.

Wakili Katuga: Waambie majaji kama mwenyekiti alisema tutahamasisha uasi.

Heche: Sijasikia.

Wakili Katuga: Waambie kama alisema mahakamani hakuendeki?

Heche: Alisema.

Wakili Katuga: Waambie Waheshimiwa Majaji kama mwenyekiti alisema polisi wanaingiza kura feki.

Heche: Alisema.

Wakili Katuga: Unajua au hujui kwamba pamoja na kesi hii, Tundu Lissu anashtakiwa kwa kutoa taarifa za uongo mtandaoni?

Heche: Sijui.

Wakili Katuga: Waambie majaji unajua au hujui kwamba mshtakiwa kwenye kesi ya Kisutu, katika hoja ya awali, alisema majaji ni ma-CCM?

Heche: Sijui.

Wakili Katuga: Unajua au hujui, ushahidi wako huu ulioutoa hapa unaweza kutumika kwenye hiyo kesi?

Heche: Sijui.

Wakili Katuga: Waambie majaji kama mwenyekiti aliwaambia au hakakuwaambia njia za kuchukua kuvuruga uchaguzi.

Heche: Yes, hakutuambia.

Wakili Katuga: Waambie majaji kama Lissu aliwaambia au hakukuwaambia njia za kuzuia uchaguzi.

Heche: Hakutuambia.

Wakili Katuga: Sema kama aliwaambia au hakuwaambia njia za kuhamasisha uasi.

Heche: Hakutuambia.

Wakili Katuga: Njia ya kukinukisha je?

Heche: Hakusema.

Wakili Katuga: Katika ushahidi wako, waambie majaji kama ulisema mwenyekiti alisema muhamasishe uasi dhidi ya nani?

Heche: Nilieleza.

Wakili Katuga: Ni ushahidi wako kwamba uasi ulikuwa uanzishwe dhidi ya Tume ya Uchaguzi?

Wakili Katuga: Waambie majaji, ni sheria ipi inayokulazimisha kwamba ukitangazwa mshindi huna uwezo wa kukataa?

Heche: Wananchi, Waheshimiwa Majaji, siyo sheria. Siijui.

Wakili Katuga: Wewe ukitangazwa kuwa mshindi, huo uchaguzi hauwi batili?

Heche: Siyo kweli.

Wakili Katuga: Ni kweli au siyo kweli uliingia bungeni kwa uchaguzi uliokuwa batili?

John Heche: Ni sahihi.

Wakili Katuga: Waambie majaji kama ni kosa au siyo kosa kama huyu mkurugenzi uliyesema alistaafu ukurugenzi wa Tume ya Uchaguzi akaenda kugombea kupitia CCM, je angekuja CHADEMA ingekuwa kosa au siyo kosa?

Wakili Katuga: Mtu yoyote aliyekuwa mtumishi wa umma, nitakuwa sahihi nikisema ana haki ya kujiunga na chama cha CHADEMA?

Heche: Ni sahihi.

Wakili Katuga: The same pia, mtu yoyote aliyemaliza utumishi wake, anaweza kujiunga na chama kingine chochote?

Heche: Hayo ni maneno yako.

Wakili Katuga: Umetaja sheria yoyote inayomkataza mtumishi wa umma kutojiunga na CCM baada ya kustaafu?

Heche: Sijataja.

Wakili Katuga: Ulisema CHADEMA mlikuwa tayari uchaguzi usogezwe mbele.

Heche: Sahihi.

Wakili Katuga: Ulisema ni sheria gani inayoruhusu uchaguzi usogezwe mbele ili kupisha mabadiliko?

Heche: Sikueleza.

Wakili Katuga: Ulisema mlienda Nairobi kumuona Raila Odinga. Waambie majaji kama kule pia mlimwambia Raila Odinga mnaenda kuzuia uchaguzi, mnaenda kukinukisha, mnaenda kuzuia uchaguzi, waambie Waheshimiwa Majaji.

Heche: Tulimwambia matatizo ya uchaguzi. Waheshimiwa Majaji, mambo tuliyoyazungumza ni yaleyale.

Wakili Katuga: Taarifa zinazotolewa na Brenda Rupia zinakuwa ni maelekezo ya chama au utashi wake binafsi?

Heche: Katibu Mkuu na ofisi yake ndiyo inamwelekeza kutoa taarifa.

Wakili Katuga: Mpaka unakuja kutoa ushahidi hapa, ulifanikiwa kusoma mashtaka au hukusoma?

Heche: Nilisoma.

Wakili Katuga: Waambie Waheshimiwa Majaji kama kuna sehemu yoyote mshtakiwa anashtakiwa kwa kuandaa mkutano?

Heche: Sijui.

Wakili Katuga: Ulisema tuhuma za mshtakiwa za kuwaalika waandishi wa habari siyo za kweli.

Heche: Sahihi.

Wakili Katuga: Kuna sehemu mshtakiwa anashtakiwa kwa kuwaalika waandishi wa habari?

Wakili Katuga: Waambie majaji kama mwenyekiti alitaka au hakutaka hotuba yake iwafikie umma?

Heche: Siwezi kukumbuka.

Wakili Katuga: Ni kweli au siyo kweli kwamba tarehe 3 Aprili 2025 kulikuwa na mkutano uliofanyika ndani huku waandishi wa habari wakiwepo?

Heche: Sikumbuki.

Wakili Katuga: Mwenyekiti alikuwa na uwezo au hakuwa na huo uwezo wa kuwaondoa au kutoongea mbele ya waandishi wa habari?

Heche: Mkutano uliandaliwa na sekretarieti. Kwa hiyo sijui.

Wakili Katuga: Ulimwona au ulimshuhudia akilazimishwa kuongea mbele ya waandishi wa habari?

Heche: Nimesema sijui.

Leave a Comment