
Waziri Mkuu Dkt. Mwigulu Nchemba amesema uwezeshaji wa wanawake wakulima ni uwekezaji katika utekelezaji wa dhana ya Afya Moja, kutokana na nafasi yao katika uzalishaji wa chakula, ufugaji, lishe, afya ya mifugo, usalama wa chakula na utunzaji wa mazingira.
“Wanawake hawapo pembezoni mwa mifumo ya chakula na kilimo; wako katikati yake. Kuwawezesha wanawake ni uwekezaji si katika kilimo pekee, bali pia katika Afya Moja,” alisema.

Dkt. Mwigulu aliyasema hayo jana, Jumatatu, Septemba 21, 2026, wakati akizungumza katika kikao cha ngazi ya juu kuhusu Mwaka wa Kimataifa wa Mwanamke Mkulima 2026, chenye mtazamo wa Afya Moja, kilichofanyika katika Kituo cha Sheikh Zayed, Makao Makuu ya Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa (FAO), jijini Roma, Italia.
Alisema Tanzania inaongozwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, ambaye ni Rais wa kwanza mwanamke katika historia ya nchi, akieleza kuwa wanawake wana nafasi kubwa katika uzalishaji wa chakula na maendeleo ya kilimo.
Hata hivyo, Dkt. Mwigulu alisema wanawake bado wanakabiliwa na changamoto za upatikanaji wa ardhi, fedha, teknolojia, huduma za ugani, masoko na nafasi za kufanya maamuzi.

BBT kuwawezesha wanawake na vijana
Waziri Mkuu alisema Serikali inaendelea kuwawezesha wanawake na vijana kupitia Mpango wa Kujenga Kesho Bora (BBT), unaolenga ifikapo mwaka 2030 kuunda ajira milioni 1.6, kusaidia biashara za kilimo 200,000 zinazomilikiwa na vijana na wanawake, pamoja na kunufaisha takribani watu milioni 10 katika vijiji 12,000.
Alisema hadi Juni 2026, kiasi cha Sh. bilioni 1.59, sawa na takribani dola za Marekani 601,000, kilikuwa kimetolewa kwa wanufaika 47, ambapo 17, sawa na asilimia 36, walikuwa wanawake.
Aidha, alisema BBT imesambaza maafisa ugani vijana 2,282 katika mikoa 22, ambao wamewafikia takribani wakulima wadogo 765,600 katika vijiji 5,856, kwa kutoa huduma za ushauri na elimu kuhusu kanuni bora za kilimo.
Serikali yawekeza katika maji na kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi
Dkt. Mwigulu alisema Serikali pia inaendelea kuwekeza katika miradi ya maji na kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi.
Alisema hadi sasa visima 395 vinavyotumia nishati ya jua na kuzingatia teknolojia zinazokabiliana na mabadiliko ya tabianchi vimechimbwa katika vijiji 234 vya wilaya 45 nchini.
Aidha, alisema Serikali inawawezesha wanawake na vijana kuhamia kutoka uzalishaji wa awali na kushiriki katika shughuli zenye thamani kubwa zaidi.
Kwa hatua hiyo, alisema vijana na wanawake 408 wamepatiwa mafunzo kuhusu uongezaji thamani wa mkonge, hatua inayolenga kuimarisha ushiriki wao katika minyororo ya thamani ya kilimo na kuongeza fursa za kipato.
“Uwekezaji huu si uwekezaji wa kilimo pekee; ni uwekezaji wa Afya Moja,” alisema.
Wanawake washirikishwe katika kufanya maamuzi
Dkt. Mwigulu alisisitiza kuwa wanawake wanapaswa kutambuliwa si kama wanufaika pekee, bali pia kama wazalishaji, wabunifu, wajasiriamali na wafanya maamuzi.
Alitoa wito wa kuimarisha sera na uwekezaji unaowawezesha wanawake kupata ardhi, fedha, teknolojia, maji, huduma za ugani na masoko.
Alisema Tanzania iko tayari kushirikiana na FAO pamoja na wadau wengine kuhakikisha Mwaka wa Kimataifa wa Mwanamke Mkulima unaacha matokeo yanayoonekana hata baada ya mwaka 2026.
ILRI: Wanawake wana nafasi muhimu katika Afya Moja
Akichangia uzoefu wake katika jopo hilo, Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Kimataifa ya Utafiti wa Mifugo (ILRI), Dkt. Appolinaire Djikeng, alisema wanawake, hususan wanawake wafugaji, tayari wana nafasi muhimu katika utekelezaji wa dhana ya Afya Moja.
Alisema wanawake wanafanya maamuzi ya kila siku kuhusu afya ya mifugo, usalama wa maji, lishe ya kaya na matumizi ya rasilimali, hivyo kutotambuliwa kwao kunaweza kudhoofisha juhudi za kudhibiti magonjwa yanayoambukizwa kutoka kwa wanyama kwenda kwa binadamu.
Dkt. Djikeng pia alisema uchambuzi wa masuala ya kijinsia haupaswi kuwa jambo la kuongezwa mwishoni katika utekelezaji wa Afya Moja, bali unapaswa kuwa sehemu ya mipango tangu mwanzo.
Alisisitiza umuhimu wa kutenga rasilimali za kutosha, ikiwemo fedha na watu, ili kuwawezesha wanawake kushiriki kikamilifu katika uongozi na kufanya maamuzi.