Watu wawili, Festo Selias Chaula na Kelvin Mhagama, wakazi wa Kata ya Tindiga, Wilaya ya Kilosa, Mkoa wa Morogoro, wamefariki dunia kwa nyakati tofauti kufuatia mzozo wa ardhi uliogeuka kuwa ghasia Septemba 23, 2026.
Wakielezea chanzo cha mkasa huo, wakazi wa vijiji vya Tindiga na Malui wamesema Chaula alivamiwa na kukatwa kwa mapanga kichwani akiwa shambani kwake baada ya kujaribu kuwazuia wafugaji kupitisha mifugo katika shamba lake, ambalo alikuwa akilitayarisha kwa ajili ya kilimo cha nyanya. Baada ya kujeruhiwa, alipelekwa katika Hospitali ya Wilaya ya Kilosa kwa matibabu, ambako alifariki dunia.
Akithibitisha kutokea kwa tukio hilo, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Morogoro, ACP Andrew Kantimbo, amesema watu wawili, Seletwi Mdamanya na Paulo Sumai, wamekamatwa kwa tuhuma za kuhusika na mauaji hayo.
Kamanda Kantimbo amesema pia askari watatu walijeruhiwa, huku gari moja pamoja na pikipiki za doria zikiharibiwa vibaya wakati wa ghasia hizo.