×

Basata Yatoa Adhabu Kwa Dudubaya na Mratibu wa Tamasha la Miaka 30 Bongo Flava -Video

Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA) limetoa adhabu kwa msanii Godfrey Tumaini maarufu Dudubaya, pamoja na Mratibu Mkuu wa Tamasha la Miaka 30 ya Bongo Flava, kufuatia tukio lililotokea Septemba 19, 2026 katika Viwanja vya General Tyre, Jijini Arusha.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na BASATA, Dudubaya anadaiwa kukiuka Kanuni ya 20(a) ya Kanuni za Baraza la Sanaa la Taifa, Tangazo la Serikali Na. 137 la tarehe 22 Mei 2026, baada ya kuzungumza maneno yaliyolalamikiwa kuwa ya kashfa na matusi wakati akitumbuiza katika tamasha hilo.

BASATA imesema baada ya kufuatilia tukio hilo na kujiridhisha kuwa kosa lilitendeka, imechukua hatua kwa mujibu wa Kanuni ya 45, ambapo Dudubaya ametakiwa:

  • Kuzingatia Sheria, Kanuni na Miiongozo ya BASATA katika uendeshaji wa sanaa.
  • Kulipa faini ya Shilingi Milioni Tatu (Tsh 3,000,000) ndani ya siku 14 kuanzia tarehe ya uamuzi.
  • Kutohusisha na shughuli za sanaa kwa jina lolote kuanzia tarehe ya uamuzi hadi pale atakapotekeleza maamuzi hayo.

MRATIBU WA TAMASHA NAYE AADHIBIWA

BASATA pia imemchukulia hatua Mratibu Mkuu wa Tamasha la Miaka 30 ya Bongo Flava, baada ya kubainika kuwa alimwezesha Dudubaya kutumbuiza jukwaani na kufanya kosa hilo licha ya kuwepo kwa masharti ya usimamizi wa tamasha.

BASATA imesema mratibu huyo alipaswa kuhakikisha kuwa shughuli za tamasha zinaendeshwa kwa kuzingatia sheria, kanuni na miongozo ya BASATA, pamoja na kuhakikisha kuwa hakuna vitendo vinavyoweza kuleta changamoto kwa wasanii wanaoshiriki.

Kwa mujibu wa Kanuni ya 45, mratibu huyo ameagizwa:

  • Kuzingatia Kanuni na Miiongozo ya BASATA katika uendeshaji wa matukio ya sanaa.
  • Kulipa faini ya Shilingi Milioni Tatu (Tsh 3,000,000) ndani ya siku 14 kuanzia tarehe ya uamuzi.
  • Kutohusisha na shughuli za sanaa kwa jina lolote kuanzia tarehe ya uamuzi hadi atakapotekeleza maamuzi hayo.

BASATA imetoa rai kwa Wasanii na Wadau wa Sanaa kuhakikisha wanazingatia Sheria, Kanuni, Miiongozo na Maadili ya Tanzania wanapotekeleza kazi zao za sanaa.

Leave a Comment