Shirika la Uwakala wa Meli Tanzania (TASAC), Ofisi ya Mkoa wa Kigoma, limekanusha taarifa zinazosambaa katika mitandao ya kijamii kuhusu kuzama kwa boti iliyodaiwa kuwa imebeba watu 40 na zaidi ya abiria 100 katika Ziwa Tanganyika.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na TASAC Septemba 25, 2026, hakuna boti iliyopakia abiria zaidi ya 100 na mizigo iliyozama kama ilivyoripotiwa.
TASAC imesema mnamo Septemba 23, 2026, majira ya saa mbili asubuhi, ilipokea taarifa kuhusu meli iliyokuwa ikiitwa MV. MJP, ambayo ilisafiri kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) ikiwa katika eneo la Mapera karibu na Bandari ya Kabimba nchini DRC.
Meli hiyo ilidaiwa kuzama majira ya saa 9 alfajiri ya Septemba 23, 2026.
Kwa mujibu wa nyaraka za meli hiyo, MV. MJP iliondoka katika Bandari ya Kigoma majira ya saa mbili usiku wa Septemba 22, 2026, ikiwa na mizigo yenye uzito wa tani 492.838, abiria 34 na mabaharia 15.
TASAC imesema imewasiliana na Mamlaka ya Udhibiti wa Usafiri Majini nchini DRC kuhusu ajali hiyo na imefafanuliwa kuwa taarifa za kuzama kwa MV. MJP ni za kweli.
Hata hivyo, TASAC imeeleza kuwa hadi kufikia Septemba 25, 2026, abiria 26 na mabaharia wote 15 walikuwa tayari wameokolewa, huku juhudi za kuwatafuta watu wengine zikiendelea.
Shirika hilo limeongeza kuwa linaendelea kushirikiana na mamlaka za DRC kufuatilia tukio hilo na kwamba taarifa nyingine zitakapotokea zitatolewa kupitia njia rasmi za mawasiliano.
TASAC imezitaka vyombo vya habari kuhakikisha vinathibitisha taarifa kutoka katika mamlaka za Serikali kabla ya kuzisambaza ili kuepusha taharuki na hofu kwa wananchi.
Aidha, TASAC imewaasa wananchi wanaotumia usafiri wa majini kufuatilia taarifa rasmi zinazotolewa na TASAC kuhusu usalama wa safari za majini.
Shirika hilo pia limewataka ITV na Millard Ayo kurekebisha taarifa walizochapisha kupitia mitandao ya kijamii ili kuondoa taharuki kwa umma.

