
Bodi ya Tumbaku Tanzania (TTB) imewakutanisha wadau wa sekta ya tumbaku nchini kujadili na kuweka mikakati ya utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 pamoja na Mpango Kabambe wa Kilimo 2050 (AMP 2050).
Kikao hicho kimewaleta pamoja wadau mbalimbali wa sekta hiyo kwa ajili ya kupitia maeneo ya kipaumbele yaliyowekwa katika Dira ya Taifa 2050 na AMP 2050, huku wakijadili namna ya kuimarisha ufuatiliaji wa utekelezaji wa shughuli na malengo ya sekta hiyo.
Akizungumza katika kikao hicho, Mkurugenzi Mkuu wa Bodi ya Tumbaku Tanzania, Stanley N. Mnozya, amesema sekta ya tumbaku ina nafasi muhimu katika kuchangia utekelezaji wa malengo ya maendeleo yaliyowekwa katika Dira ya Taifa 2050 na Mpango Kabambe wa Kilimo 2050.
Amesema maeneo yanayohitaji kupewa kipaumbele ni pamoja na kuongeza uzalishaji na tija, matumizi ya teknolojia za kisasa, uhifadhi wa mazingira, uwekezaji, kuongeza thamani ya mazao pamoja na kuendeleza rasilimali watu.
“Uzalishaji, tija, uhifadhi wa mazingira, uwekezaji, matumizi ya teknolojia za kisasa, kuongeza thamani ya mazao pamoja na maendeleo ya rasilimali watu ni miongoni mwa maeneo ambayo sekta ya tumbaku imepewa kipaumbele,” amesema Mnozya.
Mkurugenzi huyo amesema kila mdau wa sekta anapaswa kusimamia kwa umakini viashiria muhimu vya utendaji (KPIs) vilivyo katika eneo lake la uwajibikaji na kuhakikisha taarifa za utekelezaji zinawasilishwa kila robo mwaka.
Amesema mfumo huo utasaidia kupima mafanikio yaliyofikiwa, kubaini changamoto na kuchukua hatua stahiki ili kuhakikisha sekta ya tumbaku inatimiza mchango wake katika maendeleo ya Taifa.
Aidha, Mnozya amesisitiza umuhimu wa ushirikiano miongoni mwa wadau wote katika kuongeza uzalishaji wenye tija, kuimarisha ushindani wa sekta, kuvutia uwekezaji, kulinda mazingira na kuongeza mchango wa tumbaku katika ukuaji wa uchumi.
Ameongeza kuwa Bodi ya Tumbaku Tanzania itaendelea kuratibu utekelezaji wa maazimio yaliyofikiwa katika kikao hicho pamoja na kufuatilia utekelezaji wa viashiria vilivyowekwa.
Kwa mujibu wa maelezo hayo, Dira ya Taifa 2050 na Mpango Kabambe wa Kilimo 2050 vinalenga kuongeza tija, ushindani, uwekezaji na matumizi ya teknolojia katika sekta za uzalishaji, ikiwemo tumbaku, katika safari ya Tanzania kuelekea uchumi wa juu wa kati wenye ushindani na ustawi endelevu.