
Dar es Salaam – Upande wa Jamhuri umeendelea kutoa hoja zake katika kesi ya uhaini, ukieleza mbele ya Mahakama Kuu kuwa ili mtu ashtakiwe kwa kosa hilo, ni lazima awe chini ya utii wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, awe ndani au nje ya nchi, pamoja na kuwepo kwa nia inayodaiwa kuhusishwa na kosa hilo.
Katika mawasilisho yake, upande wa Jamhuri umeieleza Mahakama kuwa hati ya mashtaka inahusisha madai kwamba mshtakiwa alikusudia kuchochea umma katika kipindi cha Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025, kwa lengo la kuitisha Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Jamhuri imeeleza kuwa katika kuandaa hati ya mashtaka, baadhi ya maneno yaliyopo kwenye kifungu cha sheria yalitafsiriwa na kuwekwa kwa namna inayolingana na ushahidi ambao upande huo ulitarajia kuutoa mahakamani.
“KUTAMKA MANENO NI KITENDO”
Upande huo umeieleza Mahakama kuwa neno manifestation katika tafsiri ya kisheria linaweza kujidhihirisha kwa njia mbalimbali, ikiwemo kusambaza maandishi au michoro, pamoja na kufanya overt act, yaani kitendo kinachoonekana.
Kwa mujibu wa Jamhuri, hati ya mashtaka inadai kuwa mshtakiwa alidhihirisha nia yake kwa kutamka maneno na kisha kuyasambaza.
Jamhuri imesisitiza kuwa kutamka maneno ni kitendo katika tafsiri ya kisheria, na hoja hiyo inapaswa kuangaliwa pamoja na vipengele vya kosa vinavyotajwa katika sheria.
Aidha, upande huo umeeleza kuwa kuchapisha au kusambaza taarifa kunahusisha kufanya taarifa hiyo ijulikane kwa umma.
NENO “PUBLIC” LAIBIWA
Katika hoja zake, Jamhuri pia imeeleza matumizi ya neno public katika hati ya mashtaka, ikisema mshtakiwa anatuhumiwa kuchochea umma na si kundi maalumu au mtu mmoja.
Kwa mujibu wa hoja hizo, dhana ya public inaweza kumaanisha kundi la watu bila kuwepo kwa idadi maalumu inayotakiwa ili kundi hilo litambuliwe kama umma.
Jamhuri imeeleza kuwa matumizi ya maneno hayo katika hati ya mashtaka yamekusudiwa kufanya maelezo ya shtaka yaendane na ushahidi uliowasilishwa.
“SERIKALI” NA LENGO LA KUITISHA
Katika sehemu nyingine ya mawasilisho, Jamhuri imeeleza kuhusu matumizi ya neno Serikali katika hati ya mashtaka.
Upande huo umesema katika muktadha wa shtaka hilo, neno Serikali limetumika kuhusisha mihimili ya utendaji, bunge na mahakama, huku ukieleza kuwa Kanuni ya Adhabu haina tafsiri mahususi ya maneno executive na judiciary katika kifungu hicho.
Jamhuri imeirejea pia sehemu ya ushahidi ambapo mshtakiwa alieleza kuwa “the executive is responsible” kwa ajili ya kutunza amani, huku jukumu la kulinda amani likihusishwa na polisi walio chini ya Serikali.
Kwa hoja ya Jamhuri, ushahidi huo unaonyesha kuwa jambo lililodaiwa kutishiwa ni Serikali katika jukumu lake la kudumisha amani na utulivu.
“SI LAZIMA KUTHIBITISHA SERIKALI ILITISHIKA”
Jamhuri imeendelea kusisitiza kuwa katika kuthibitisha shtaka, si lazima ionyeshe kwamba Serikali kweli ilitishwa au ilitikisika kutokana na maneno yanayodaiwa kutolewa na mshtakiwa.
Kwa mujibu wa hoja hizo, kinachotakiwa kuangaliwa ni iwapo kulikuwa na nia ya kuitisha Serikali kama inavyodaiwa katika hati ya mashtaka.
Upande wa Jamhuri pia umebainisha kuwa baadhi ya maneno yaliyotumika katika hati ya mashtaka yametokana na vifungu vya sheria, huku mengine yakichaguliwa ili kuendana na mazingira ya ushahidi uliowasilishwa.
Baada ya kukamilisha hoja zake kuhusu masuala hayo, Jamhuri imeendelea kuielekeza Mahakama kwenye vipengele viwili vinavyohusiana na iwapo mshtakiwa alikuwa na nia ya kuitisha Serikali na iwapo matendo yanayodaiwa yanaendana na masharti ya kosa la uhaini.
Kesi hiyo inaendelea mbele ya jopo la Majaji watatu la Mahakama Kuu.