×

TANAPA Yasitisha Njia Mbili za Kupanda Mlima Kilimanjaro Baada ya Moto

Mamlaka ya Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA) imesitisha kwa muda matumizi ya njia za Lemosho na Londorosi zinazotumiwa na watalii kupanda Mlima Kilimanjaro, kufuatia kuzuka kwa moto mpya wa porini ndani ya Hifadhi ya Taifa ya Kilimanjaro.

Kwa mujibu wa taarifa ya TANAPA, moto huo umeibuka katika eneo la Sangarini-Kamwanga na unaelekea upande wa Shira ndani ya hifadhi hiyo.

Kutokana na hali hiyo, watalii waliokuwa wamepanga kutumia njia za Lemosho na Londorosi wataelekezwa kutumia njia nyingine, ambazo ni Machame, Marangu au Rongai, hadi hapo hali ya moto itakapokuwa imedhibitiwa.

TANAPA imesema juhudi za kuuzima moto huo zinaendelea kwa ushirikiano na Jeshi la Zimamoto na Uokoaji, Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania, Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori ya Enduimet, vikosi vya akiba, wananchi wa maeneo yanayozunguka hifadhi pamoja na wadau wengine wa utalii.

Moto huo umeibuka wiki chache baada ya moto mwingine kuripotiwa Septemba 3 katika eneo la Kikererwa, karibu na mpaka wa Tanzania na Kenya. Moto huo wa awali ulidhibitiwa kwa zaidi ya asilimia 90 kufikia Septemba 5.

TANAPA imeeleza kuwa usalama wa watumishi, watalii na wadau wengine unaendelea kuwa kipaumbele, huku rasilimali zilizopo zikielekezwa katika juhudi za kudhibiti na kuzima moto huo.

Leave a Comment