
Bangkok, Thailand — Tukio la kushtua limetokea nchini Thailand baada ya gari la umeme kuvamia eneo la hekalu na kuwagonga waabudu waliokuwa wamekaa mbele ya madhabahu ya Kibudha.
Video iliyosambaa mtandaoni inaonyesha gari aina ya sedan ya rangi ya kijivu likipenya kwa kasi ndani ya eneo la Guanyin Shrine, katika kituo cha Thian Fah Foundation jijini Bangkok.
Kwa mujibu wa taarifa za awali, gari hilo lilikuwa likiendeshwa na mwanaume mwenye umri wa miaka 78. Ghafla, gari hilo lilipoteza mwelekeo na kuvamia eneo ambalo lilikuwa limejaa watu waliokuwa wamekaa mbele ya madhabahu.
Tukio hilo lilitokea majira ya saa 7 mchana siku ya Alhamisi, na polisi waliitwa baada ya kupokea taarifa kuhusu ajali hiyo kubwa.

Picha za video zinaonyesha watu waliokuwapo wakikimbia kwa hofu huku wengine wakikimbilia kuwasaidia waathirika wa ajali hiyo.
Watu watatu walijeruhiwa katika tukio hilo na walipatiwa msaada baada ya ajali.
Mamlaka zinaendelea kuchunguza chanzo cha dereva huyo kupoteza udhibiti wa gari na kuingia ndani ya eneo la hekalu.
Video ya tukio hilo imezua mshtuko mkubwa kutokana na namna gari hilo lilivyoingia ghafla katika eneo lililokuwa na waabudu wengi.