×

Naomi Campbell Ashinda Kesi, Kuendelea Kuongoza Taasisi za Misaada

LONDON, UINGEREZA: Mwanamitindo maarufu duniani, Naomi Campbell, ameshinda kesi ya kupinga marufuku ya miaka mitano iliyokuwa imemzuia kuhudumu kama mdhamini wa taasisi za misaada nchini England na Wales.

Uamuzi huo umetolewa Alhamisi na mahakama maalumu yenye majaji watatu, ambao walibaini kuwa Campbell, mwenye umri wa miaka 56, alipotoshwa na Bianka Hellmich, aliyekuwa mdhamini mwenzake katika taasisi ya Fashion for Relief.

Miaka miwili iliyopita, Charity Commission, taasisi inayosajili na kusimamia mashirika ya misaada nchini England na Wales, ilibaini kuwepo kwa matukio kadhaa ya utovu wa nidhamu na usimamizi mbaya katika Fashion for Relief.

Miongoni mwa masuala yaliyoibuliwa ni matumizi ya fedha za taasisi kugharamia baadhi ya matumizi binafsi ya Campbell, ikiwemo malazi katika hoteli ya nyota tano mjini Cannes, huduma za spa, room service pamoja na sigara.

Kutokana na matokeo hayo, Charity Commission ilimwekea Campbell marufuku ya miaka mitano ya kuhudumu kama mdhamini wa taasisi ya misaada.

Katika uamuzi wake mpya, mahakama imethibitisha kuwa kulikuwa na utovu mkubwa wa nidhamu na usimamizi mbaya ndani ya taasisi hiyo.

Hata hivyo, majaji walihitimisha kuwa matatizo katika usimamizi wa fedha na matumizi mabaya ya fedha za taasisi yalitokana na vitendo vya Hellmich, ambavyo vilifichwa kutoka kwa Campbell.

Mahakama ilibaini pia kuwa Hellmich alitumia nyaraka za kughushi na aliwapotosha washauri wa kitaalamu pamoja na Charity Commission.

Majaji walikubaliana kwamba Campbell alishiriki kwa kiwango fulani katika kushindwa kwa taasisi hiyo kuwasilisha hesabu zake kwa wakati. Hata hivyo, walisema jambo hilo pekee halikumfanyi kuwa mtu asiyefaa kuhudumu kama mdhamini wa taasisi ya misaada.

Wakati wa kusikilizwa kwa kesi hiyo kwa siku nne mwezi Juni, Campbell alisema kosa lake pekee lilikuwa kumwamini Hellmich, ambaye alimfahamu kama mwanasheria.

Campbell pia alidai kuwa Hellmich alighushi saini yake na kutoa taarifa zisizo za kweli kuhusu sifa zake za kitaaluma.

Akizungumza mbele ya mahakama hiyo iliyopo London, Campbell alisema hakuliona tukio hilo kama kushindwa kwake, bali kama matokeo ya kumwamini mtu aliyedhani anaweza kumtegemea.

Charity Commission ilikuwa imepinga ombi la Campbell na kutaka marufuku ya miaka mitano iendelee kutumika.

Uchunguzi wa Fashion for Relief ulianzishwa na Charity Commission mwaka 2021 baada ya kuibuka kwa maswali kuhusu usimamizi wa taasisi hiyo.

Fashion for Relief, ambayo Campbell alihusishwa nayo, iliandaa matukio ya kuchangisha fedha mjini Cannes na London kwa ajili ya kusaidia miradi ya kupambana na umaskini.

Baada ya uchunguzi, taasisi hiyo ilivunjwa na kuondolewa kwenye rejista rasmi ya mashirika ya misaada nchini England na Wales mwaka 2024.

Uamuzi wa mahakama sasa unamruhusu Naomi Campbell kuendelea kuwa na uwezo wa kuhudumu kama mdhamini wa taasisi za misaada nchini England na Wales, huku mahakama ikitofautisha wajibu wake na vitendo vya usimamizi vilivyofanywa na Hellmich.

Leave a Comment