×

Chivayo na Mkewe Kuzikwa Bila Kuonyeshwa Miili, Familia Yafunguka

Familia ya mfanyabiashara wa Zimbabwe, Wicknell Chivayo, imesema hakutakuwa na utaratibu wa kuonyeshwa miili ya marehemu Chivayo na mke wake, Lulu, kabla ya mazishi kutokana na hali ya miili yao baada ya ajali ya helikopta iliyowaua.

Msemaji wa familia, Hebert Chivayo, amesema miili ya wanandoa hao ilipata madhara makubwa katika ajali hiyo, huku sehemu za miili yao zikitawanyika katika eneo la tukio.

Akizungumza na waombolezaji waliokusanyika katika makazi ya marehemu Ijumaa jioni, Hebert amesema hali hiyo imefanya familia kuamua kutokuwa na utaratibu wa kuonyeshwa miili wakati wa mazishi.

Amesema wataalamu wa uchunguzi wa kisayansi bado wanaendelea na vipimo vya DNA kwa ajili ya kutambua na kutenganisha mabaki ya waathirika, kabla ya familia kuendelea na maandalizi ya mazishi.

Hadi sasa, familia haijatangaza tarehe rasmi ya mazishi.

Chivayo, ambaye baada ya kifo chake alitangazwa kuwa shujaa wa mkoa na Rais wa Zimbabwe, Emmerson Mnangagwa, alifariki Jumatano pamoja na mke wake na abiria wengine baada ya helikopta waliyokuwa wakisafiria kuanguka katika eneo la vijijini la Marondera.

Familia inaendelea kusubiri kukamilika kwa mchakato wa utambuzi wa mabaki kabla ya kutangaza mipango zaidi kuhusu mazishi.

Leave a Comment