×

Absa yaahidi Kuboresha Huduma kwa Kusikiliza Maoni ya Wateja

DAR ES SALAAM: Absa Bank Tanzania imeahidi kuendelea kuboresha huduma zake kwa kuzingatia maoni na mahitaji ya wateja, huku ikisisitiza umuhimu wa kwenda hatua ya ziada katika kuwahudumia.

Ahadi hiyo imetolewa wakati benki hiyo ikizindua rasmi Wiki ya Huduma kwa Wateja 2026, yenye kaulimbiu ya “Extra Mile”, inayolenga kuhamasisha wafanyakazi kuongeza ubora na ufanisi katika utoaji wa huduma.

Akizungumza katika hafla hiyo, Mkurugenzi Mtendaji wa Absa Bank Tanzania, Obedi Laiser, amesema wateja wanahitaji zaidi ya bidhaa za kifedha, bali pia uzoefu mzuri katika kila hatua ya mwingiliano wao na benki.

Amesema kila mteja ana mahitaji, malengo na changamoto zake, hivyo wafanyakazi wanapaswa kusikiliza kwa makini, kuitikia kwa wakati na kuwajibika katika kutafuta suluhisho.

“Kila mteja ana hadithi yake, na kila mwingiliano tunaokuwa nao na mteja huyo unakuwa sehemu ya hadithi hiyo. Absa, ahadi ya chapa yetu ni rahisi: ‘Story yako ina Thamani’,” amesema Laiser.

Laiser amesema kwenda hatua ya ziada hakumaanishi kufanya mambo makubwa pekee, bali pia kuhakikisha huduma zinatolewa kwa haraka, ufanisi na kwa kuzingatia mahitaji ya kila mteja.

Amesema benki hiyo itaendelea kutafuta uwiano kati ya matumizi ya teknolojia na mwingiliano wa kibinadamu, kutokana na mabadiliko ya matarajio ya wateja katika huduma za kifedha.

Katika hafla hiyo, Absa pia imewatambua wafanyakazi kutoka vitengo mbalimbali kwa mchango wao katika kuboresha huduma kwa wateja, wakiwemo wale wanaofanya kazi nyuma ya pazia kuhakikisha huduma zinaendelea kutolewa kwa ufanisi.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Wateja Binafsi wa Absa Bank Tanzania, Ndabu Lilian Swere, amesema maoni yatakayokusanywa kutoka kwa wateja wakati wa wiki hiyo yatatumika kubaini maeneo yanayohitaji maboresho.

Katika hatua nyingine, mteja wa muda mrefu wa benki hiyo, Hilary Biduga, ameitaka Benki Kuu ya Tanzania pamoja na mamlaka husika kuangalia suala la ukomo wa umri katika utoaji wa mikopo, akisema baadhi ya wateja wenye umri mkubwa bado wana uwezo mkubwa wa kifedha na kuendesha biashara.

Biduga amesema tathmini ya uwezo wa mteja kurejesha mkopo inapaswa pia kuzingatiwa badala ya kutegemea umri pekee.

Absa imesisitiza kuwa dhana ya “Extra Mile” haipaswi kuishia katika Wiki ya Huduma kwa Wateja, bali iwe sehemu ya utamaduni wa kila siku wa benki katika kuhakikisha wateja wanapata huduma bora.

Leave a Comment