
DAR ES SALAAM: Tukio la kushtua limetokea Mtaa wa Senzele, Kata ya Bunju B, jijini Dar es Salaam, baada ya Laurent Kweka kudaiwa kumuua mkewe, Jeni Urassa, kwa kumpiga risasi kichwani na kisha kujisalimisha kwa Polisi.
Tukio hilo linadaiwa kutokea Alhamisi, Oktoba 1, 2026, majira ya saa 11:30 alfajiri, ndani ya nyumba walimokuwa wakiishi wanandoa hao.
Kaimu Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Faustine Mafwele, amethibitisha kutokea kwa tukio hilo na kusema mtuhumiwa anashikiliwa na Polisi kwa ajili ya upelelezi.
Kwa mujibu wa Mafwele, Laurent na marehemu Jeni walikuwa wanandoa na wote walitoka mkoani Kilimanjaro.

Amesema baada ya uchunguzi kukamilika pamoja na taratibu nyingine za kisheria, mtuhumiwa atafikishwa mahakamani.
Mgogoro wa nyumba wadaiwa kuchangia
Mfanyakazi wa ndani wa familia hiyo, Rebecca Mbasha, ambaye amesema amefanya kazi katika nyumba hiyo kwa takribani miaka minane, amedai kuwa mauaji hayo yalitokana na mgogoro wa muda mrefu wa kifamilia kuhusu umiliki wa nyumba.
Rebecca amesema Jeni alikuwa akitaka kubadilisha majina yaliyokuwa kwenye hati ya nyumba ili kubakiza jina lake pamoja na majina ya watoto wao.
Kwa mujibu wa Rebecca, Jeni alieleza kuwa yeye ndiye aliyenunua kiwanja na kujenga nyumba hiyo.
Akisimulia kinachodaiwa kutokea siku ya tukio, Rebecca amesema Laurent aliingia nyumbani na muda mfupi baadaye alimsikia Jeni, kisha akasikia kishindo.
Amesema aliporejea ndani ya nyumba, alimkuta Laurent akitoka chumbani akiwa ameshika bastola na kumwambia, “nimeshamaliza kazi.”
Rebecca amesema alipoingia chumbani alimkuta Jeni akiwa ameanguka chini akiwa na jeraha kichwani.
Aliwahi kutishiwa kwa bastola
Jacqueline Nkaya, ambaye ni mama mdogo wa marehemu, amesema wanandoa hao walikuwa na mgogoro wa muda mrefu.
Amedai kuwa wakati mmoja Jeni aliwahi kutishiwa kuuawa kwa kutumia bastola na mumewe na kwamba tukio hilo liliripotiwa Polisi.
Jacqueline amesema Laurent aliondoka Dar es Salaam na kwenda mkoani Kilimanjaro, ambako alikaa kwa takribani miezi miwili kabla ya kurejea jijini siku ya tukio.
Hata hivyo, majirani wa familia hiyo wamesema hawakuwa na taarifa kuhusu kuwepo kwa migogoro hiyo, wakieleza kuwa kwa nje familia hiyo ilionekana kuishi kwa amani tangu ilipohamia katika nyumba hiyo Desemba 2025.
Marehemu Jeni ameacha watoto wanne, watatu wakiwa wanafunzi na mmoja ambaye bado hajaanza shule.
Polisi wanaendelea na uchunguzi wa tukio hilo, huku Laurent akiendelea kushikiliwa kwa mujibu wa taratibu za kisheria.