ARUSHA: Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, ameyataka mabunge kuimarisha usimamizi wa rasilimali za umma na uwajibikaji wa serikali, akisisitiza umuhimu wa kuhakikisha maslahi na mahitaji ya wananchi yanazingatiwa katika maamuzi.
Rais Samia ametoa ujumbe huo kupitia picha mjongeo iliyoonyeshwa wakati wa ufunguzi wa Mkutano wa 153 wa Umoja wa Mabunge Duniani (IPU), uliofanyika Oktoba 5, 2026 katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa Arusha (AICC).
Katika ufunguzi huo, Rais Samia aliwakilishwa na Waziri Mkuu, Dkt. Mwigulu Nchemba, katika mkutano unaofanyika kuanzia Oktoba 5 hadi 9, 2026.

Rais Samia amesema mamlaka ya mabunge yanatokana na wananchi, hivyo yana wajibu wa kutunga sheria kwa maslahi ya umma, kuchunguza mgawanyo na matumizi ya rasilimali za taifa pamoja na kuiwajibisha serikali.
Amesema Serikali yake inaheshimu nafasi ya Bunge katika kuisimamia na kuishauri Serikali, akieleza kuwa usimamizi huo una mchango katika kuimarisha utendaji na uwajibikaji kwa wananchi.

Aidha, Rais Samia amesema kaulimbiu ya mkutano huo inayohusu kuimarisha utawala bora na kuziwezesha jamii kupitia ushirikishwaji, kuaminiana na fursa kwa wote inaendana na changamoto zinazoikabili dunia kwa sasa.
Amehimiza mabunge kutathmini makubaliano yanayofikiwa na serikali pamoja na kuendeleza ushirikiano unaovuka tofauti za kisiasa na mipaka ya nchi.
Kwa upande wake, Waziri Mkuu Dkt. Mwigulu Nchemba amesema mabunge yana nafasi muhimu katika kuhakikisha taasisi za umma zinaitikia mahitaji ya wananchi kupitia utungaji wa sheria, uidhinishaji wa matumizi ya fedha na usimamizi wa shughuli za serikali.

Dkt. Mwigulu ametaja kuimarishwa kwa Ofisi ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), ambayo imetengewa zaidi ya Shilingi bilioni 132 katika mwaka wa fedha 2026/2027, kuwa miongoni mwa hatua za kuimarisha usimamizi wa rasilimali za umma.
Amesema Rais Samia anaamini katika utawala wa kikatiba na mgawanyo wa madaraka, akisisitiza umuhimu wa kuwa na taasisi imara na huru katika kujenga jamii yenye ustawi, utulivu na ushirikishwaji.
