×

Stanbic Yaahidi Kuwafungulia Wateja Milango Ya Fursa Katika Wiki Ya Huduma Kwa Wateja

Dar es Salaam, Tanzania, Jumatatu tarehe 5 Oktoba 2026. Benki ya Stanbic Tanzania leo imezindua Wiki ya Huduma kwa Wateja 2026 kwa kuonyesha mabadiliko ambayo wateja wake tayari wanayatumia, badala ya ahadi kuhusu huduma. Kubwa kuliko yote ni uwezo wa kuwalipa wasambazaji wa biashara wa China moja kwa moja kwa kutumia sarafu ya Yuan, jambo linalorahisisha hatua ya kubadilisha fedha katika kila malipo anayofanya mfanyabiashara wa Tanzania na China.

Hadi mwaka jana, mfanyabiashara wa Kariakoo aliyetaka kumlipa msambazaji wake wa Guangzhou alilazimika kupitisha fedha zake katika dola za Marekani kabla hazijabadilishwa kuwa Yuan.

Tangu Agosti mwaka huu, wateja wa Stanbic wanalipa moja kwa moja kwa Yuan. Malipo yanafika haraka, usumbufu umepungua, na mfanyabiashara anaepuka gharama ya kubadilisha fedha mara mbili, jambo linalolinda faida yake na bei anazowauzia wateja wake.

China ndiyo nchi inayoongoza kuuza bidhaa Tanzania. Mwaka jana pekee, bidhaa zenye thamani ya dola za Marekani bilioni 8.17 ziliingia nchini kutoka China.

Akizungumza katika Tawi la Stanbic Ubungo jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi Mtendaji wa benki hiyo, Manzi Rwegasira, alisema kauli mbiu ya mwaka huu, Hatua ya Ziada, inapimwa katika huduma ya kila siku na si katika mradi mmoja, na kwamba ongezeko la wateja wa benki linathibitisha hilo.

“Ongezeko la wateja wetu limeanza kuonekana, na linaisaidia biashara nzima. Lakini takwimu ni matokeo, si chanzo. Ni kitu muhimu mnachoyafanya kila siku kuwahudumia wateja ndiyo kinayoleta tofauti. Kuna siku mvua inanyesha, kuna siku jua linawaka na joto ni kali, na bado mnafika kazini. Hiyo ndiyo hatua ya ziada.”   Manzi Rwegasira

“Wateja wetu wameibeba benki hii kwa zaidi ya miongo mitatu. Wiki hii tunawashukuru, na tunaahidi kuendelea kwenda mbali zaidi kwa ajili yao. Tanzania ni nyumbani kwetu, na tunachochea ukuaji wake.”   alimaliza kusema,  Manzi Rwegasira,  Mtendaji Mkuu, Benki ya Stanbic Tanzania

Benki inasema mabadiliko haya yametokana na kuwasikiliza wateja, na yameonekana katika maeneo matatu: biashara ya kimataifa, ukuzaji wa ujasiriamali, na huduma za kila siku za kibenki. Mbali na malipo kwa yuan, zaidi ya wajasiriamali 5,000 wamepata mafunzo na ushauri kupitia Stanbic Biashara Incubator, na biashara zaidi ya 600 ndogo na za kati zimeunganishwa na kampuni kubwa kama wasambazaji.

Zaidi ya nusu ya biashara hizo zinaongozwa na wanawake. Hapa nyumbani, mteja sasa anaweza kufungua akaunti na kupokea malipo kwa simu yake, bila kulazimika kufika tawini.

Mkuu wa Idara ya Wateja Binafsi na Wateja Maalumu, Omari Mtiga, alisema kauli mbiu hiyo lazima ionekane katika matendo ya kila siku ili iwe na maana zaidi ya wiki moja.

“Kwangu, kwenda hatua ya ziada kuna maana ya mambo matatu: kusikiliza zaidi, kujali zaidi, na kuwajibika zaidi. Wateja hawatarajii kuhudumiwa tu. Wanatarajia kueleweka. Mteja haoni idara wala kitengo. Anamwona mtu, na kile anachofanya mtu huyo ndicho kinachokuwa taswira ya benki akilini mwake.”  Omari Mtiga, Mkuu wa Idara ya Wateja Binafsi na Wateja Maalumu, Benki ya Stanbic Tanzania

Mkuu  wa Kitengo cha Huduma kwa Wateja, Benki ya Stanbic Tanzania, Lilian Abdulmalik, anayesimamia ajenda ya huduma ndani ya benki, alisema wiki hii imeandaliwa ili ipimwe kwa yale yatakayofuata. Shughuli za wiki hii zitafanyika katika matawi yote ya Stanbic nchini kote, ambapo timu zitawatembelea wateja katika maeneo yao ya biashara na viongozi waandamizi watakutana na wateja matawini kila siku.

“Wiki hii tunawaendea wateja wetu badala ya kuwasubiri. Lakini kiwango tunachojiwekea wiki hii ndicho tunachotaka kukidumisha katika kila tawi, kila wiki ya mwaka. Huduma si idara ndani ya Stanbic. Ni jinsi kila mmoja wetu anavyojitokeza kwa ajili ya wanaotubanki nasi.”   Lilian Abdulmalik, Mkuu wa Kitengo cha Huduma kwa Wateja, Benki ya Stanbic Tanzania

Wiki hii itahitimishwa siku ya Ijumaa katika Hospitali ya Vijibweni, ambapo benki itafanya shughuli ya uwekezaji wa kijamii kama sehemu ya kuendelea kuunga mkono sekta ya afya katika jamii inazozihudumia.

“Tunaihitimisha wiki hii katika Hospitali ya Vijibweni kwa sababu kuwahudumia wateja vizuri na kuihudumia jamii vizuri ni ahadi ile ile. Kwenda hatua ya ziada hakuwezi kuishia mlangoni mwa tawi. Benki ni sehemu ya jamii inayoifanyia kazi, na tunapowekeza katika kituo kama Vijibweni, tunawekeza kwa familia zile zile zinazotuamini na maisha yao.”  — Lilian Abdulmalik

Leave a Comment