
Mwanamuziki mkongwe wa muziki wa dansi nchini Tanzania, Gaby Kababa Nkomba, amefariki dunia jijini Stockholm, Sweden, Oktoba 5, 2026.
Taarifa za kifo chake zimetolewa na Kiongozi wa Bendi ya Dekula, Dekula Kahanda, ambaye amesema Kababa amefariki Oktoba 5, bila kutoa maelezo zaidi kuhusu chanzo cha kifo.
Kababa Nkomba alikuwa miongoni mwa magwiji wa muziki wa dansi nchini Tanzania na mmoja wa waanzilishi wa bendi ya Safari Sound iliyokuwa maarufu nchini katika miaka ya 1970.
Kabla ya kuwa sehemu ya Safari Sound, Kababa aliwahi kuitumikia bendi ya OSS iliyojulikana kwa mtindo wa Nyekesee Paralizee.
Baadaye alitumikia mtindo wa Masantula chini ya uongozi wa King Kikii, kabla ya kujiunga na mtindo wa Dukuduku uliokuwa chini ya uongozi wa Ndala Kasheba.
Kababa alihamia nchini Sweden mwaka 1984, ambako aliendelea na shughuli za muziki na baadaye kuwa mwimbaji katika Dekula Band.
Katika kipindi cha hivi karibuni, Kababa alikuwa sehemu ya Dekula Band na alishiriki katika kazi mbalimbali za muziki. Miongoni mwa kazi zake za mwisho ni wimbo “Didier”, uliotolewa kwenye albamu Opika! ya Dekula Band, huku video yake ikipatikana kupitia YouTube.
Kifo cha Kababa Nkomba kimeacha pengo katika muziki wa dansi, hasa kutokana na mchango wake katika historia na maendeleo ya muziki huo nchini Tanzania.
Familia, ndugu, marafiki na wadau wa muziki wa dansi wameendelea kuomboleza msiba huo.
Poleni sana familia ya muziki wa dansi kwa msiba huu.