
ARUSHA: Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Mwigulu Nchemba, amefanya mazungumzo na Makamu Mwenyekiti wa Bunge la Vietnam, Nguyen Hong Dien, katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa Arusha (AICC).
Mazungumzo hayo yamefanyika Oktoba 5, 2026, kando ya Mkutano wa 153 wa Umoja wa Mabunge Duniani (IPU) unaofanyika jijini Arusha.

Katika mazungumzo hayo, viongozi hao wamejadili namna ya kuimarisha uhusiano wa Tanzania na Vietnam pamoja na kupanua maeneo ya ushirikiano kati ya nchi hizo mbili.
Miongoni mwa maeneo yaliyojadiliwa ni ushirikiano wa kiuchumi, kisiasa na kijamii, kwa lengo la kuongeza manufaa kwa wananchi wa Tanzania na Vietnam.

Mkutano huo ni sehemu ya mikutano ya viongozi mbalimbali wanaoshiriki Mkutano wa 153 wa IPU, unaozikutanisha nchi mbalimbali duniani kujadili masuala yanayohusu mabunge, utawala bora na ushirikiano wa kimataifa.
