DAR ES SALAAM — Rais wa Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS), Wakili Boniface Mwabukusi, amemtaka Msajili wa Vyama vya Siasa nchini, Jaji Francis Mutungi, kuvifuatilia vyama vya siasa ambavyo havionekani kutekeleza majukumu na shughuli zao kikamilifu, akipendekeza vifutwe iwapo havikidhi matakwa ya kisheria.
Mwabukusi ametoa kauli hiyo leo, Oktoba 7, 2026, wakati wa uzinduzi wa uongozi mpya na nembo ya Baraza la Vyama vya Siasa, uliofanyika katika Hoteli ya Hyatt Regency jijini Dar es Salaam.
Amesema ni muhimu Msajili kuhakikisha vyama vya siasa vilivyosajiliwa vinafanya shughuli zao kwa mujibu wa sheria na taratibu zilizowekwa, badala ya kubaki kwenye orodha ya vyama vilivyosajiliwa bila kuwa na shughuli zinazoonekana.
Aidha, Mwabukusi amesisitiza umuhimu wa kutoa nafasi kwa kizazi kipya, hususan vijana wa Gen Z, kushiriki kikamilifu katika shughuli za kisiasa nchini.
Amesema vijana hao wanapaswa pia kupewa fursa ya kuanzisha vyama vyao vya siasa iwapo wanaona kuna haja ya kuwa na majukwaa yatakayowakilisha mitazamo na matarajio ya kizazi chao.
Kwa mujibu wa Mwabukusi, ushiriki wa vijana katika siasa ni muhimu katika kuhakikisha mifumo ya kisiasa inaendelea kuakisi mabadiliko ya kijamii na mitazamo ya vizazi vipya.