×

Familia ya Urassa Yakataa Ukoo wa Kweka Kufika Nyumbani Kwao Kuaga Mwili wa Jane – Video

HAI, KILIMANJARO: Familia ya Urassa imesema haitaruhusu watu wa ukoo wa Kweka kufika nyumbani kwao katika Kijiji cha Nkuu Sinde, Wilaya ya Hai, mkoani Kilimanjaro, wakati wa shughuli za kuaga mwili wa Jane Urassa, ikieleza kuwa wanaotaka kumuaga wataruhusiwa kufanya hivyo wakati wa ibada ya kanisani pekee.

Msimamo huo umetolewa na msemaji wa familia hiyo, Judica Urassa, leo Ijumaa, Oktoba 9, 2026, wakati mwili wa Jane ulipowasili nyumbani kwao kwa ajili ya shughuli za kuaga kabla ya mazishi.

Akizungumza na waombolezaji waliokusanyika nyumbani hapo, Judica amewataka kuwa waangalifu katika kauli zao na kuepuka kuzungumzia mambo ambayo hawana ufahamu nayo.

“Mtu asiongee kitu asichokijua na asiongee chochote. Wapo askari msiowajua na mnaowajua, hivyo mnaweza kuongea na kujikuta mnalala sehemu msiyoijua,” amesema Judica.

Amesisitiza kuwa familia ya marehemu haina nafasi kwa ukoo wa Kweka kufika nyumbani kwao wakati wa shughuli hizo, akieleza kuwa utaratibu uliowekwa ni kwa wanaotaka kumuaga Jane kukutana kanisani wakati wa ibada.

“Watu wa ukoo wa Kweka hatuwahitaji hapa nyumbani. Ikiwa wanataka kuaga, tukutane kanisani, lakini hapa nyumbani hapana,” amesema.

Mwili wa Jane Urassa uliwasili nyumbani kwa wazazi wake saa 2:45 asubuhi katika Kijiji cha Nkuu Sinde, Kata ya Machame Mashariki, Wilaya ya Hai, kwa ajili ya shughuli za kuuaga kabla ya mazishi.

Msimamo huo wa familia umewekwa wazi wakati wa maandalizi ya kumuaga marehemu, huku familia ikielekeza kuwa ibada ya kanisani ndiyo itakayokuwa fursa kwa wanaotaka kumuaga Jane, wakiwemo watu wa ukoo wa Kweka.

Hata hivyo, taarifa iliyotolewa haijaeleza sababu za kina za kutoruhusu ukoo wa Kweka kufika nyumbani kwa familia ya Urassa wakati wa shughuli hizo.

Leave a Comment