×

Serikali, Vodacom Tanzania Foundation Waongeza Upatikanaji wa Mafunzo ya Kidijitali kwa Walimu

Maelfu ya walimu nchini sasa watanufaika na upatikanaji wa mafunzo ya maendeleo ya kitaaluma kupitia matumizi ya teknolojia, hatua inayolenga kuongeza umahiri wa ufundishaji, kuongeza ufaulu wa wanafunzi na kuchochea maendeleo ya taifa kupitia elimu.

Mafanikio hayo yanatokana na ushirikiano kati ya Taasisi ya Elimu Tanzania (TIE) na Vodacom Tanzania Foundation katika utekelezaji wa Programu ya Mafunzo Endelevu ya Walimu Kazini (TCPD/MEWAKA), ambayo imeimarisha matumizi ya Mfumo wa Usimamizi wa Kujifunza (LMS) pamoja na Vituo vya Rasilimali za Walimu (TRC) nchini.

Akizungumza wakati wa hafla ya kukabidhi na kuzindua kituo cha Rasilimali za Walimu kilichojengwa shule ya Msingi Naurei, wilayani Arusha, kikiwa ni cha kwanza kati ya 50 vinavyotarajiwa kujengwa hapa nchini, Mkuu wa wilaya ya Arumeru Neema Lugangira alisema uwekezaji kwa walimu ni uwekezaji wa moja kwa moja katika kuongeza uwezo wa kufundisha kwa kutumia TEHAMA, na kwa ujumla mustakabali wa elimu nchini.

“Leo nimekuja kuzindua kituo hiki, hili sio jambo dogo maana kituo hiki kitaongeza ubora wa elimu hapa nchini, na pia ni uthibitisho kwamba serikali na sekta binafsi zikishirikiana kuimarisha miundombinu, teknolojia na mifumo inayomwezesha mwalimu kujifunza na kujiendeleza wakati wote matokeo yake ni kuboresha elimu kwa ujumla wake. Mwalimu anayepata maarifa mapya, anayeongeza kiwango cha elimu alichonacho na kutumia teknolojia kwa ufanisi, huongeza nafasi ya wanafunzi kufaulu na kufikia ndoto zao,” alisema Mh Lugangira.

Alisema tathmini ya mahitaji ya TCPD/MEWAKA iliyohusisha Vituo vya Rasilimali za Walimu 178, walimu 350 na wadau mbalimbali imebaini kuwa walimu wengi wana hamasa ya kujifunza na kutumia teknolojia, huku asilimia 99 wakifahamu LMS na asilimia 71 wakiwa na uelewa wa msingi wa TEHAMA.

Hata hivyo, tathmini hiyo imeonesha kuwa changamoto za upatikanaji wa vifaa vya TEHAMA, kompyuta, intaneti na usaidizi wa kiufundi bado zinaendelea kuathiri matumizi kamili ya mfumo huo, hasa katika maeneo ya vijijini.

“Mafanikio ya TCPD/MEWAKA hayategemei motisha ya mwalimu pekee. Yanahitaji uwekezaji katika vifaa, uwepo wa intaneti, mafunzo ya vitendo na mifumo imara. Ndio maana ushirikiano kati ya serikali na sekta binafsi una umuhimu mkubwa katika kuhakikisha walimu wanapata mazingira bora ya kujifunza,” alisisitiza.

Mkuu wa Wilaya pia aliipongeza Vodacom Tanzania Foundation kwa mchango wake katika kuendeleza elimu nchini na kuzihamasisha taasisi nyingine za sekta binafsi kuunga mkono juhudi hizo.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Vodacom Tanzania Foundation, Zuweina Farah alisema uwekezaji katika walimu ni moja ya njia zinazoleta matokeo makubwa katika kuboresha mfumo wa elimu na kukuza uchumi wa kidijitali wa taifa.

“Tunafahamu kuwa walimu ndiyo nguzo ya maendeleo ya elimu. Wanapopewa fursa za kujifunza na kutumia teknolojia kwa ufanisi, matokeo chanya huonekana moja kwa moja kwa wanafunzi na jamii kwa ujumla. Hii ndiyo sababu Vodacom Tanzania Foundation imeamua kuwekeza katika mifumo na miundombinu inayowezesha maendeleo ya walimu kwa njia endelevu,” alisema Farah.

Aliongeza kuwa kupitia ushirikiano na TIE, matumizi ya LMS yameondolewa gharama za data kwa watumiaji wa mtandao wa Vodacom, hatua iliyolenga kupunguza vikwazo vya upatikanaji wa maudhui ya maendeleo ya kitaaluma kwa walimu.

“Kupitia ushirikiano wetu na TIE, walimu wanaotumia mtandao wa Vodacom wanaweza kuifikia LMS bila gharama yeyote. Tunaamini teknolojia ina uwezo mkubwa wa kuondoa vikwazo vya upatikanaji wa elimu na kuhakikisha walimu wengi zaidi wanapata fursa ya kuendeleza taaluma zao bila kujali mahali walipo,” alisema.

Farah aliongeza kuwa sekta binafsi inaweza kuharakisha utekelezaji wa mipango ya elimu kwa kuwekeza katika teknolojia, muunganisho wa intaneti, vifaa vya TEHAMA, ubunifu na utaalamu wa kidijitali unaohitajika ili kujenga mfumo wa elimu unaoendana na mahitaji ya karne ya 21.

 

Leave a Comment