×

Aucho Aaga Timu ya Taifa ya Uganda, Acha Historia Ya Mechi 77

Nahodha wa zamani wa timu ya taifa ya Uganda, Khalid Aucho, ametangaza kustaafu kuichezea timu hiyo ya taifa, Uganda Cranes, baada ya kuitumikia kwa miaka 13 katika soka la kimataifa.

Katika taarifa yake rasmi iliyotolewa Oktoba 12, 2026, Aucho amesema amefikia uamuzi huo baada ya safari ndefu iliyompa heshima ya kuwakilisha nchi yake, kucheza michezo 77 na hatimaye kuvaa kitambaa cha unahodha wa timu ya taifa.

Aucho, ambaye alianza kuitumikia Uganda Cranes Novemba 30, 2013, amesema kucheza akiwa amevaa jezi yenye rangi za bendera ya nchi yake, nyeusi, njano na nyekundu, imekuwa moja ya heshima kubwa zaidi katika maisha yake.

Amesema moja ya mafanikio makubwa katika safari yake ya soka ni kuwa sehemu ya timu iliyosaidia Uganda kufuzu kwa fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON), baada ya kusubiri kwa miaka 38. Pia ameitumikia nchi hiyo katika mashindano matatu ya AFCON na kupata nafasi ya kuiongoza timu akiwa nahodha.

Katika taarifa hiyo, Aucho amewashukuru Shirikisho la Soka Uganda (FUFA), viongozi wa soka, makocha wake, wachezaji wenzake na mashabiki kwa mchango wao katika safari yake. Miongoni mwa makocha aliowataja ni Milutin “Micho” Sredojević, Sébastien Desabre, Johnathan McKinstry na Paul Put, huku akitoa heshima maalumu kwa marehemu Fred Kajoba.

Licha ya kustaafu kuichezea timu ya taifa, Aucho amesema bado ataendelea kuiunga mkono soka la Uganda na ana imani kizazi kipya cha wachezaji kitaendeleza historia ya Uganda Cranes. Amehitimisha kwa kueleza kuwa anaondoka akiwa na shukrani, fahari na upendo mkubwa kwa nchi yake.

Leave a Comment