×

Waziri Sangu Azindua Msimu wa Semina Za Wastaafu Watarajiwa Wa Psssf

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu – Kazi, Ajira na Mahusiano, Deus Sangu, akizungumza kwenye Semina ya Maandalizi ya Kustaafu alipofanya ufunguzi wa Semina hiyo katika ukumbi Ukumbi wa Jjegoen Park Sumbawanga Mkoani Rukwa.

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu – Kazi, Ajira na Mahusiano, Mhe. Deus Sangu, ameipongeza Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kuimarisha mifuko ya hifadhi ya jamii na kuboresha utoaji wa huduma kwa wanachama na wastaafu, hususan katika ulipaji wa mafao kwa wakati.

Mhe. Sangu ameyasema hayo Oktoba 12, 2026, mjini Sumbawanga, mkoani Rukwa, wakati akizindua msimu wa semina za kuwaandaa wastaafu watarajiwa wa Mfuko wa Hifadhi ya Jamii kwa Watumishi wa Umma (PSSSF) kwa kipindi cha mwaka 2026/2028.
Akizungumza katika uzinduzi huo, Waziri Sangu amesema mafanikio yaliyopatikana katika kuimarisha mifuko ya hifadhi ya jamii ni pamoja na ulipaji wa mafao kwa wakati, kuendelea kulipa madeni ya mifuko hiyo na kuboresha kiwango cha chini cha pensheni kwa wastaafu.

Mstaafu mtarajiwa Bw. Mohamed Suleiman Lugoya akiuliza swali wakati wa Semina ya Maandalizi ya Kustaafu iliyofanyika katika Ukumbi wa Jjegoen Park Sumbawanga Mkoani Rukwa

“Kwa kweli tuna kila sababu ya kumpongeza Rais wetu kwa kuhakikisha mifuko ya hifadhi ya jamii ikiwemo PSSSF inaimarika. Hivi sasa mafao yanalipwa kwa wakati, Serikali inaendelea kulipa madeni yake kwa mifuko ya hifadhi ya jamii, pensheni za kila mwezi zinalipwa kwa wakati, na kiwango cha chini cha pensheni kimeboreshwa. Hakika, hayo ni mafanikio makubwa ya Serikali ya Awamu ya Sita,” amesema Mhe. Sangu.
Ameongeza kuwa, kiwango cha chini cha pensheni kwa wastaafu kimefikia Shilingi 250,000 kwa mwezi, akieleza kuwa hatua hiyo ni miongoni mwa maboresho yaliyofanywa na Serikali kwa lengo la kuimarisha ustawi wa wastaafu.

Akizungumzia umuhimu wa semina hizo, ambazo zitafanyika katika mikoa ya Mwanza, Arusha, Dar es Salaam na Dodoma pamoja na Unguja kwa upande wa Zanzibar, Mhe. Sangu ameipongeza PSSSF kwa kuandaa mafunzo yanayolenga kuwaandaa watumishi wanaokaribia kustaafu kukabiliana na maisha baada ya kumaliza utumishi wa umma.

 

Afisa Matekelezo wa Mfuko wa PSSSF Bw. Frank Fute wakitoa mada wakati wa Semina ya Maandalizi ya Kustaafu iliyofanyika katika ukumbi wa Jjaggoen Park Sumbawanga Mkoani Rukwa, Leo tarehe 12 Octoba 2026.

“Ninawapongeza PSSSF kwa kuandaa semina hizi ambazo zinazinduliwa leo. Hakika, haya ni mafunzo muhimu yanayowaandaa wastaafu watarajiwa kuishi maisha bora baada ya kustaafu. Hongereni sana PSSSF, na ninawasihi semina hizi ziwe endelevu,” amesema.

Akizungumzia kaulimbiu ya PSSSF ya ‘Tunalipa Jana’, Waziri Sangu amesema kaulimbiu hiyo inaakisi utekelezaji wa huduma za Mfuko katika kulipa mafao kwa wakati, akiwahimiza wastaafu watarajiwa kuwa na imani na Mfuko huo.

“Kulipa Jana si nadharia, ni ukweli mtupu, na wengi wameshathibitisha hilo. Shukrani za pekee ziende kwa Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuiwezesha PSSSF kulipa jana. Hivyo, kuweni na amani kwani PSSSF ipo tayari kuwalipa,” amesema.

Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Rukwa, Mhe. Makongoro Nyerere, akitoa salamu za mkoa, ameitaka PSSSF kuendelea kuwa karibu na wastaafu na kuhakikisha wanapata mafao yao kwa usahihi na kwa wakati, akisisitiza kuwa Mfuko huo unapaswa kuwa chanzo cha faraja na uhakika kwa wanachama wake wanapomaliza utumishi.

Naye Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa PSSSF, Bw. Paul Kijazi, amesema kuwa hadi Juni 30, 2026, Mfuko ulikuwa umelipa jumla ya wanachama 390,761 mafao yenye thamani ya Shilingi trilioni 12.94.
Amesema PSSSF inaendelea kuimarisha mifumo yake ya utoaji huduma ili kuhakikisha wanachama wanaostahili wanapata mafao yao kwa wakati, akibainisha kuwa kaulimbiu ya ‘Tunalipa Jana’ inaendelea kuwa sehemu muhimu ya juhudi za Mfuko katika kuboresha huduma kwa wanachama na wastaafu.
Akifafanua kuhusu maudhui ya semina hizo, Bw. Kijazi amesema washiriki watapatiwa elimu kuhusu usimamizi wa fedha na fursa mbalimbali za uwekezaji, ikiwemo uwekezaji katika viwanda vidogo na vya kati kulingana na uwezo wao, masoko ya fedha, kilimo-biashara na ujasiriamali.
Amesema mafunzo hayo yanalenga kuwasaidia wastaafu watarajiwa kufanya maamuzi sahihi kuhusu matumizi na uwekezaji wa mafao yao, ili yaweze kuwapatia manufaa ya muda mrefu na kuwawezesha kukabiliana na mahitaji ya maisha baada ya kustaafu.

Semina hizo zinawezeshwa na wadau mbalimbali, wakiwemo Azania Bank, NMB Bank, CRDB Bank, Amana Bank, Orbit Security, UTT, Watumishi Housing investment,, Absa Bank na NBC Bank, ambao wanatoa elimu na mwongozo kuhusu huduma za kifedha na fursa za uwekezaji kwa wastaafu watarajiwa wa PSSSF.

Mkuu wa Mkoa wa Rukwa, Mhe. Makongoro Nyerere kwenye picha ya pamoja na Viongozi wa Mfuko wa PSSSF walipotembelea Ofisi ya Mkuu wa Mkoa.

Leave a Comment