×

Mfanyabiashara Bunju Afikishwa Mahakamani kwa Tuhuma za Kumuua Mkewe kwa Kumpiga Risasi

DAR ES SALAAM: Mfanyabiashara Laurence Kweka, mwenye umri wa miaka 48 na mkazi wa Bunju A, jijini Dar es Salaam, amefikishwa katika Mahakama ya Wilaya ya Kinondoni akikabiliwa na shtaka la kumuua mkewe, Jane Maloo Urassa, kwa kumpiga risasi.

Kweka amefikishwa mahakamani leo Alhamisi, Oktoba 15, 2026, ambapo Wakili wa Serikali, Harrison Lukosi, amemsomea shtaka hilo mbele ya Hakimu Mkazi Mwandamizi, Kemilembe Josiah.

Kwa mujibu wa maelezo ya shtaka yaliyosomwa mahakamani hapo, mshtakiwa anadaiwa kutenda kosa hilo Oktoba 1, 2026, katika eneo la Bunju A, Wilaya ya Kinondoni, mkoani Dar es Salaam, kwa kumuua Jane Maloo Urassa.

Shtaka hilo linasikilizwa katika kesi ya mauaji namba 23407 ya mwaka 2026 na linahusishwa na vifungu vya 196 na 197 vya Sheria ya Kanuni ya Adhabu, Sura ya 16, iliyofanyiwa marejeo mwaka 2023.

Hata hivyo, Kweka hakutakiwa kujibu shtaka hilo baada ya Hakimu Josiah kumweleza kuwa Mahakama ya Wilaya ya Kinondoni haina mamlaka ya kusikiliza kesi za mauaji.

Aidha, mahakama hiyo imemweleza mshtakiwa kuwa shtaka la mauaji analokabiliwa nalo halina dhamana kwa mujibu wa sheria, hivyo ataendelea kusalia rumande wakati upelelezi wa shauri hilo ukiendelea hadi utakapokamilika.

Kesi hiyo inahusu tuhuma za mauaji zinazodaiwa kutokea katika eneo la Bunju A, jijini Dar es Salaam, na hatua zaidi za kisheria zitasubiri kukamilika kwa upelelezi.

Leave a Comment