
Miss Grand International 2026, Jihan Dimack, amemshukuru Mfanyabiashara Jennifer Jovin ‘Niffer’ kwa upendo na sapoti kubwa aliyompa wakati wa mashindano hayo, akisema mchango wake ulimvuka matarajio na kumfanya ajisikie kupendwa na kuungwa mkono kwa namna ya kipekee.
Jihan amesema hakutarajia kuingia katika Top 8 kwenye kipengele cha Country’s Power of the Year hadi pale Niffer alipojitokeza kuhamasisha viongozi, wasanii na wananchi kupiga kura, hatua iliyochochea mshikamano mkubwa miongoni mwa Watanzania.

Kupitia ujumbe wake wa shukrani, Jihan ameeleza kuwa licha ya kutowahi kukutana ana kwa ana na Niffer, upendo na kujitoa kwake wakati wa mashindano hayo vimemgusa kwa kiwango kikubwa.
“Dear Niffer, mpenzi wangu! Hatujawahi kukutana, lakini upendo na sapoti uliyonimiminia ni zaidi ya maneno yanavyoweza kueleza au dunia kuelewa. Mungu alikutumia na katika mchakato huo ulisimama nami kwa upendo. Asante sana Niffer! Nakupenda sana na siwezi kusubiri kukuona,” ameandika Jihan.
Aidha, Jihan amefichua kuwa amekuwa akimpenda Niffer kwa muda mrefu na alikuwa shabiki wake, akisema anashangazwa na namna Mungu alivyowaunganisha kupitia safari hiyo ya mashindano.

“Nimekuwa nikikupenda siku zote na nilikuwa shabiki wako, lakini leo angalia jinsi Mungu alivyotuunganisha. Kwa mara nyingine, asante sana kwa kila kitu. Tutaonana hivi karibuni!” ameongeza Jihan.
Akijibu ujumbe huo, Niffer ameeleza kufurahishwa na namna Jihan anavyoendelea kumthamini, huku akikiri kuwa hajazoea kupokea maneno ya shukrani yenye hisia kama hayo.
“Eeeh wewe Jihan jamani, unapendeka sana kipenzi changu! Tena post nyingine ya shukrani. Sijazoea binadamu wenye moyo mwema kama huu jamani. Asante mpenzi wangu, nakupenda sana mno, na familia ya Niffer inakupenda sana! Sote tunakupenda sana na hatuwezi kusubiri kukuona,” ameandika Niffer.

Amehitimisha ujumbe wake kwa dua na matamko ya upendo, akisema: “Mungu atubariki sana, sana, sana! Tunakupenda sana!”
Majibizano hayo ya upendo na shukrani yameibua hisia mbalimbali kwa mashabiki kwenye mitandao ya kijamii, wengi wakimpongeza Niffer kwa kujitoa kwake wakati wa upigaji kura na kuhamasisha Watanzania kuiunga mkono Jihan.
Baadhi ya mashabiki pia wametaka watu wengine waliochangia katika safari hiyo, akiwemo Pharm Solomon, watambuliwe kwa juhudi zao za kuwaelekeza Watanzania namna ya kupiga kura na kufuatilia hatua za mashindano.
Ingawa Jihan hakufanikiwa kushinda kipengele cha Country’s Power of the Year na kuishia nafasi ya pili, ameonyesha kuthamini mshikamano alioupata kutoka kwa Watanzania, huku uhusiano wake na Niffer ukiendelea kuwa gumzo kutokana na namna ulivyojengwa kupitia upendo, kujitoa na sapoti wakati wa mashindano hayo.