
DAR ES SALAAM: Mashabiki wa urembo nchini Tanzania wameonyesha hamasa kubwa kuelekea kuwasili kwa Jihan Dimack, mshindi wa taji la Miss Grand International 2026, huku maandalizi ya kumpokea yakiendelea kuvuta hisia za wananchi na watumiaji wa mitandao ya kijamii.
Jihan anatarajiwa kuwasili nchini kupitia Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA), Terminal 3, jijini Dar es Salaam ambako mashabiki wameeleza shauku ya kumpokea kwa furaha kufuatia mafanikio yake katika mashindano hayo ya kimataifa ya urembo.

Kupitia ukurasa wake wa Instagram, Jihan alituma ujumbe wa kuashiria kurejea nyumbani akisema, “TANZANIAAAAAAAA, I’m coming home”, akimaanisha kuwa anarudi nyumbani Tanzania.
Aidha, aliwashukuru watu wa Thailand kwa upendo na ushirikiano alioupata tangu siku ya kwanza, pamoja na vyombo vya habari vilivyompa nafasi ya kutangaza safari yake ya ushindani.
Katika ujumbe wake, Jihan alisema anathamini upendo aliooneshwa na kueleza kuwa anatarajia kurejea tena Thailand siku zijazo.

Miongoni mwa waliomkaribisha kwa ujumbe wa pongezi ni Jokate Mwegelo, aliyeandika, “Welcome home our mega star”, akimaanisha, “Karibu nyumbani, nyota wetu mkubwa.”
Maoni ya mashabiki kwenye mitandao ya kijamii yameendelea kuonesha furaha na fahari, huku wengi wakimuita malkia wao na kumpongeza kwa mafanikio hayo. Baadhi yao wameandika, “Karibu sana malkia wetu,” huku wengine wakieleza kuwa wanamsubiri kwa hamu.

BURUDANI DAR VILLAGE
Wakati huo huo, Mfanyabiashara Jennifer Jovin ‘Niffer’ amewahamasisha Watanzania kujitokeza kwa wingi kumpokea Jihan na kutakuwa na tukio la burudani linalotarajiwa kufanyika leo katika ukumbi wa Dar Village baada ya mapokezi hayo. Mapokezi hayo ya Jihan yataishiaka katika Mall ya Dar Village.

MISS GRAND INTERNATIONAL YAFIKISHA VIEWS BILIONI 2.33
Umaarufu wa Miss Grand International 2026 umeonekana pia katika mitandao ya kijamii, baada ya waandaaji kutangaza kuwa mashindano hayo yamekusanya jumla ya watazamaji zaidi ya bilioni 2.33 katika majukwaa mbalimbali kwa kipindi cha Septemba 18 hadi Oktoba 16, 2026.
Kwa mujibu wa takwimu zilizowekwa kwenye bango rasmi la mashindano hayo, Instagram imeongoza kwa kupata watazamaji bilioni 1.4, ikifuatiwa na TikTok yenye milioni 581.7, Facebook yenye milioni 334 na YouTube yenye milioni 22.5.

Takwimu hizo zinaonesha ukubwa wa mwitikio wa mashindano hayo katika majukwaa ya kidijitali na nafasi ya mitandao ya kijamii katika kufikisha maudhui ya mashindano ya urembo kwa hadhira ya kimataifa.
Kwa Tanzania, ushindi wa Jihan Dimack umeongeza hamasa na fahari miongoni mwa mashabiki wa urembo, ambao sasa wanatarajia kumpokea mshindi huyo nyumbani na kusherehekea mafanikio yake katika jukwaa la kimataifa.