×

Polisi Wamkamata Mama Anayedaiwa Kutapeli Kwa Kisingizio cha Kutoa Taarifa Za Uongo

Jeshi la Polisi Mkoa wa Arusha linamshikilia Vivian Jackson Salekwa, mkazi wa Majengo jijini Arusha, kwa tuhuma za kutoa taarifa za uongo kuhusu kutekwa kwake, akidaiwa kulenga kutisha familia yake ili kupata fedha.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Jeshi la Polisi Mkoa wa Arusha Oktoba 18, 2026, tukio hilo lilitokea Oktoba 10, 2026, ambapo mtuhumiwa alidaiwa kuondoka nyumbani na kutoweka bila familia yake kujua alikokwenda.

Baada ya taarifa za kutoweka kwake kupokelewa, uchunguzi ulianza kubaini chanzo na mazingira ya tukio hilo. Hata hivyo, Oktoba 16, 2026, mtuhumiwa alibainika kuwa mzima na kudaiwa kujifanya ametekwa ili familia yake iamini kuwa yuko hatarini na kumtafuta.

Polisi wameeleza kuwa Vivian alidaiwa kutuma ujumbe kwa mfanyakazi wake, Mariam Mwinjuma, akimtaka awasilishe taarifa hizo za uongo kwa wazazi wake ili waamini kuwa ametekwa na kujificha.

Jeshi la Polisi limesema mtuhumiwa huyo anaendelea kushikiliwa pamoja na Mariam Mwinjuma na Castus Bagambisa, ambaye ni mpenzi wake, kwa ajili ya taratibu nyingine za kisheria.

Katika taarifa hiyo, Polisi wameonya dhidi ya tabia ya kutoa au kusambaza taarifa za uongo zinazoweza kusababisha taharuki katika jamii, wakisisitiza kuwa kufanya hivyo ni kinyume cha sheria na hatua za kisheria zitachukuliwa dhidi ya wahusika.

Aidha, Jeshi la Polisi Mkoa wa Arusha linaendelea na uchunguzi kuhusu tukio jingine la mtu mmoja anayedaiwa kuingia kwa nguvu katika nyumba ya wageni iliyopo eneo la Kaloleni jijini Arusha, usiku wa kuamkia Oktoba 18, 2026.

Polisi wamewataka wananchi kuendelea kushirikiana na vyombo vya usalama kwa kutoa taarifa sahihi zitakazosaidia kudumisha amani na usalama katika jamii.


Leave a Comment