
Ujenzi wa barabara jijini Mbeya umeanza kushika kasi siku chache baada ya Makamu wa Rais, Deogratius Ndejembi, kutoa maelekezo ya kuharakishwa kwa kazi hiyo, huku maeneo yaliyokuwa na changamoto ya upitaji yakianza kufunguliwa ili kupunguza usumbufu kwa wananchi na wafanyabiashara.
Akizungumzia utekelezaji wa maelekezo hayo, Meneja wa Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) Mkoa wa Mbeya, Mhandisi Suleiman Bishanga, amesema hatua mbalimbali zimechukuliwa kufungua njia zinazotumiwa na wananchi wakati ujenzi ukiendelea.
Bishanga amesema eneo la Kabwe ni miongoni mwa maeneo yanayotekelezwa katika mradi wa ujenzi wa barabara kutoka Sadaka kuelekea Physical 29, ambapo juhudi zinaendelea kuhakikisha wananchi wanapata njia za kupita kwa urahisi.
“Tumetambua jumla ya maeneo 116 kuanzia Msagala hadi Fisi ambayo yalihitaji kufunguliwa ili wananchi waweze kupita. Maeneo hayo tumeshayafungua na sasa tunaendelea kuyaboresha ili yaweze kupitika bila shida,” amesema.

Ameongeza kuwa mkandarasi ameagizwa kufanya kazi usiku na mchana ili kuongeza kasi ya utekelezaji wa mradi na kuhakikisha viwango vya ubora vinazingatiwa. Amesema kazi za kuweka saruji zinaendelea katika maeneo husika, huku lengo likiwa ni kukamilisha mradi na kupunguza usumbufu kwa wananchi na wafanyabiashara.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Mbeya ambaye pia ni Mbunge wa Mbeya Mjini, Patrick Mwalunenge, amesema ameridhishwa na kasi ya ujenzi baada ya kutembelea maeneo ya mradi na kujionea kazi zinazotekelezwa chini ya usimamizi wa TANROADS na mkandarasi.
Mwalunenge amesema kasi ya kazi imeongezeka na baadhi ya njia zinazotumiwa na wafanyabiashara na wasafirishaji zimeanza kufunguliwa. Ametolea mfano eneo la Mdope, ambako vifusi vimewekwa ili kurahisisha magari kuingia na kutoka katika maeneo ya biashara.
Amesema kukamilika kwa barabara hiyo kutachochea shughuli za kiuchumi jijini Mbeya kwa kurahisisha usafirishaji wa bidhaa, kuongeza ufanisi wa biashara na kuboresha mwonekano wa jiji.
Aidha, amewataka wananchi kuendelea kuwa na imani na Serikali inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan, akieleza kuwa mradi huo ni sehemu ya jitihada za kuboresha miundombinu na kurahisisha huduma za usafiri.
Mwalunenge pia amewataka wasimamizi wa mradi kuhakikisha maeneo ya biashara yanaendelea kufikika wakati ujenzi ukiendelea. Ameshauri sehemu ambazo bado hazijawekewa lami zimwagiwe maji ili kupunguza vumbi linaloweza kuwaathiri wafanyabiashara na watumiaji wa barabara.
Akizungumzia hali iliyokuwepo kabla ya kutolewa kwa maelekezo ya Makamu wa Rais, mkazi wa Mbeya, Amos John, amesema baadhi ya njia za mitaa zilikuwa na changamoto kubwa ya upitaji, hali iliyosababisha bajaji, bodaboda na magari kupata ugumu wa kufika katika maeneo mbalimbali.
Hata hivyo, amesema baada ya maelekezo hayo, baadhi ya njia zimeanza kufunguliwa na kuwekwa vifusi, hatua ambayo imerahisisha usafirishaji na kupunguza usumbufu kwa watumiaji wa barabara hizo.
Naye Emanuel Mwakalinga, anayefanya shughuli zake katika eneo la Mdope, karibu na vibao vya Shule ya Rwanda Nzovwe, amesema ameshuhudia kasi ya maendeleo ya ujenzi huo, akibainisha kuwa uwekaji wa vifusi umeboresha upitaji wa magari na kurahisisha upatikanaji wa maeneo ya biashara.
Mwakalinga amesema hatua za kufungua njia zinazounganisha mitaa na barabara kuu zimeanza kuwasaidia wananchi waliokuwa wakipata changamoto ya kufika katika maeneo yao ya shughuli za kiuchumi.
Wananchi hao wameishukuru Serikali kwa kuendelea kutekeleza mradi huo na kupongeza maelekezo ya Makamu wa Rais, wakieleza matumaini yao kuwa kukamilika kwa barabara hiyo kutarahisisha usafiri, kuchochea biashara na kuimarisha maendeleo ya kiuchumi jijini Mbeya.