
Jengo la ghorofa nyingi lililokuwa likijengwa limeporomoka katika eneo la Eastleigh, Nairobi nchini Kenya, na kuzua hofu ya watu kunasa kwenye vifusi.
Tukio hilo limetokea kando ya Barabara ya 9 leo Oktoba 23, 2026, ambapo wahudumu wa dharura, polisi na maafisa wa usalama wamewasili kuanza shughuli za uokoaji na kudhibiti hali katika eneo hilo.
Serikali ya Kaunti ya Nairobi imetuma mashine maalumu kusaidia kuondoa vifusi na kurahisisha juhudi za kuwafikia watu ambao huenda wamenasa. Wakati huohuo, juhudi za kutafuta rasilimali zaidi za kusaidia operesheni hiyo zinaendelea.

Maafisa wa Shirika la Msalaba Mwekundu la Kenya na Jeshi la Ulinzi la Kenya (KDF) pia wameripotiwa kufika eneo la tukio kusaidia shughuli za uokoaji. Msalaba Mwekundu umewataka wananchi kukaa mbali na eneo hilo ili kutoa nafasi kwa wahudumu wa dharura kutekeleza majukumu yao kwa usalama.
Hofu imeongezeka kutokana na taarifa kwamba ghorofa ya chini na ya kwanza ya jengo hilo zilikuwa na maduka, hali inayozua wasiwasi kuhusu usalama wa wafanyabiashara, wateja na wapita njia waliokuwa katika eneo hilo wakati wa tukio.

Mkuu wa Polisi wa Nairobi, Issa Mohamed, amesema mamlaka zilikuwa zikisubiri taarifa zaidi huku maafisa wa polisi wakiongezwa kusaidia kuratibu shughuli za uokoaji. Jengo hilo limeporomoka takribani saa 7 mchana, wakati eneo la Eastleigh huwa na shughuli nyingi za kibiashara.

Kwa mujibu wa mashuhuda, kulikuwa na vurugu katika eneo la tukio, huku baadhi ya watu wakiripotiwa kurusha mawe dhidi ya ambulansi na kuzilazimisha kubadili njia kwa muda. Polisi waliofika eneo hilo walitumia mabomu ya machozi kuwatawanya watu waliokuwa wamekusanyika.
Hadi sasa, chanzo cha kuporomoka kwa jengo hilo na idadi ya watu waliojeruhiwa, kufariki au kunasa kwenye vifusi haijathibitishwa. Shughuli za uokoaji zinaendelea huku mamlaka zikijitahidi kubaini ukubwa wa maafa hayo.