
MBEYA — Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya limeendelea kushirikiana na wananchi na wadau mbalimbali katika kuimarisha ulinzi na usalama wa maisha na mali za wananchi, huku likitoa taarifa kuhusu mauaji ya mwanamke, kukamatwa kwa watuhumiwa wa uhalifu na hatua zilizochukuliwa dhidi ya waandamanaji na madereva waliokiuka sheria.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya Oktoba 22, 2026, mnamo Oktoba 16, 2026, saa 11:45 alfajiri, katika Mtaa wa Makunguru, Kata ya Ruanda, Tarafa ya Iyunga, Jiji la Mbeya, Nice Kabuye, mhudumu wa nyumba ya kulala wageni ijulikanayo kwa jina la Igogwe, alitoa taarifa kwa Kituo cha Polisi Mbeya Mjini kuwa chumba kimoja katika nyumba hiyo kilichopewa jina la Uphilipino kilikutwa na miili ya watu wawili, mwanamke na mwanaume, wakiwa wamefariki dunia na kufichwa uvunguni mwa kitanda.
Baada ya kupokea taarifa hiyo, Jeshi la Polisi lilifika eneo la tukio na kuanza uchunguzi. Mwili mmoja ulitambuliwa kuwa wa Annastazia Mwakipesile (32), aliyekuwa mkazi wa Kabwe, huku mwili wa mwanaume mwingine ukiwa haujatambuliwa hadi wakati taarifa hiyo inatolewa. Mwili huo ulihifadhiwa katika Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Mbeya.
Mnamo Oktoba 21, 2026, saa 9 alasiri, Jeshi la Polisi lilifanikiwa kumkamata mtuhumiwa Benson Steven, maarufu kwa jina la Mk embo, fundi sofa na mkazi wa Iyamba, Jiji la Mbeya, kwa tuhuma za kuhusika na mauaji hayo.
Uchunguzi wa awali umebaini kuwa chanzo cha tukio hilo ni imani za kishirikina zinazohusishwa na kutafuta utajiri. Kwa mujibu wa taarifa hiyo, mtuhumiwa alikiri kwa hiari yake kuwa aliongozwa na imani hizo na alidai kwenda kwa mganga wa jadi aliyempa masharti ya kufanya mauaji ili apate utajiri.
Taarifa hiyo inaeleza kuwa mtuhumiwa alipokuwa akipelekwa kwa mganga huyo, aliruka ghafla kutoka kwenye gari na kuanza kukimbia. Askari aliyekuwa akimfuatilia alifyatua risasi tatu hewani kwa lengo la kumtahadharisha na kumtaka asimame, lakini aliendelea kukimbia hadi alipofyatuliwa risasi iliyompata katika paja la mguu wa kushoto.
Mtuhumiwa alipelekwa katika Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Mbeya kwa matibabu kutokana na jeraha alilopata, lakini alifariki dunia akiwa anaendelea kupatiwa matibabu.
Aidha, kumbukumbu zinaonyesha kuwa Benson Steven aliwahi kukamatwa Temeke, Dar es Salaam, kwa tuhuma za kuvunja nyumba usiku na kuiba. Alitiwa hatiani na kufungwa jela mwaka mmoja, kisha baada ya kumaliza kifungo chake alifika Mbeya. Pia, mnamo Desemba 29, 2025, alikamatwa akiwa na wenzake wanane na kufikishwa mahakamani kwa kesi ya unyang’anyi wa kutumia silaha. Waliachiwa huru baada ya mlalamikaji kuugua na kushindwa kufika mahakamani kutoa ushahidi.
MADEREVA 19 NA BAJAJI 19 WAKAMATWA KWA KUKIUKA SHERIA
Katika hatua nyingine, Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya limeendelea kutekeleza agizo la Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Jumanne Sagini, kuhusu kukabiliana na madereva wanaokiuka sheria za usalama barabarani.
Mnamo Oktoba 19, 2026, saa 8 mchana, polisi walianza kusimamia utekelezaji wa maagizo hayo kwa kufanya misako na doria iliyowezesha kuwakamata madereva 19 na bajaji 19 waliokuwa wakifanya fujo na kukiuka sheria za usalama barabarani. Watuhumiwa hao walifikishwa katika Kituo cha Polisi Mwanjelwa kwa hatua zaidi za kisheria.
Oktoba 20, 2026, madereva 18 walifikishwa katika Mahakama ya Mwanzo Mbeya Mjini na kushitakiwa kwa kufanya fujo. Walitiwa hatiani na kuhukumiwa kifungo cha miezi mmoja jela. Watuhumiwa wengine wanane walifikishwa mahakamani kwa kosa la kuharibu mali baada ya kuvunja vioo vya mabasi na daladala 11, huku kesi yao ikiendelea kusikilizwa.
Katika mwendelezo wa matukio hayo, Oktoba 20, 2026, makundi mbalimbali ya vijana yaliendelea kufanya fujo na kufunga barabara katika maeneo ya Nane Nane. Katika matukio hayo, vijana watano walikamatwa na Oktoba 21, 2026, walifikishwa Mahakama ya Mwanzo Mbeya Mjini. Mshitakiwa mmoja alikiri kosa na kuhukumiwa kifungo cha mwezi mmoja jela, huku kesi za watuhumiwa wengine wanne zikiendelea kusikilizwa.
WATUHUMIWA 15 WA FUJO WAFIKISHWA MAHAKAMANI
Mnamo Oktoba 21, 2026, saa 9 alasiri, Mbunge wa Jimbo la Mbeya Mjini, Patrick Mwalanenge, alikutana na maafisa wa usafirishaji waliokuwa na madai yasiyo halali ya kutaka kwenda kuwatolea gerezani watuhumiwa waliokamatwa na kufungwa kutokana na matukio ya fujo.
Jeshi la Polisi liliwatawanya na kuwakamata wagomaji na waandamanaji 15 waliokuwa wakifanya fujo. Oktoba 22, 2026, watuhumiwa hao walifikishwa Mahakama ya Mwanzo Mbeya Mjini, ambapo 11 walitiwa hatiani na kuhukumiwa kifungo cha miezi minne jela au kulipa faini ya Shilingi 400,000 kila mmoja.
Watuhumiwa wengine wanne walikiri makosa yao na kuhukumiwa kifungo cha mwezi mmoja jela au kulipa faini ya Shilingi 200,000 kila mmoja.
POLISI WATOA ONYO
Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya limetoa wito kwa wananchi wenye tamaa ya kujipatia fedha na mali kwa njia zisizo halali kuacha mara moja vitendo vya uhalifu, likisisitiza kuwa uhalifu haulipi na hauna nafasi katika jamii.
Aidha, polisi limewataka wananchi kuacha kujiingiza katika vitendo vya fujo na uvunjifu wa amani, kwa kuwa vinaweza kusababisha madhara makubwa kwa watu na mali zao.
Taarifa imetolewa na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya, Oktoba 22, 2026.