×

TMA Yatoa Tahadhari ya Mafuriko, Yaweka Wazi Utabiri wa Mvua

Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) imetabiri mvua za wastani hadi juu ya wastani katika maeneo mbalimbali nchini kwa msimu wa mvua wa Novemba 2026 hadi Aprili 2027, huku ikitoa tahadhari kuhusu athari zinazoweza kujitokeza, zikiwemo mafuriko, magonjwa ya mlipuko na uharibifu wa miundombinu.

Katika utabiri wake uliotolewa Oktoba 23, 2026, TMA imeeleza kuwa mvua nyingi zaidi zinatarajiwa katika kipindi cha Novemba 2026 hadi Januari 2027, ikilinganishwa na miezi ya Februari hadi Aprili mwaka ujao.

Mkurugenzi wa TMA, Dk. Ladslaus Chang’a, amesema mwenendo huo wa mvua unatarajiwa kuchangiwa kwa kiasi kikubwa na hali ya El Niño yenye nguvu kubwa, inayohusishwa na ongezeko la joto la bahari katika eneo la tropiki ya kati ya Bahari ya Pasifiki.

Amesisitiza kuwa wananchi na wadau wa sekta mbalimbali wanapaswa kuendelea kufuatilia taarifa za hali ya hewa zinazotolewa kila siku, kila baada ya siku 10 na kila mwezi, ili kupata utabiri unaoendana na mabadiliko ya hali ya hewa katika maeneo yao.

Kwa mujibu wa utabiri huo, mikoa ya Kigoma, Tabora, Katavi, Singida, Dodoma, Njombe, Iringa, Mbeya, Songwe na Rukwa, pamoja na maeneo ya kusini mwa Mkoa wa Morogoro, inatarajiwa kupata mvua za juu ya wastani hadi wastani.

Wakati huohuo, mikoa ya Ruvuma, Mtwara na Lindi inatarajiwa kupata mvua za wastani hadi juu ya wastani katika kipindi hicho.

TMA imeeleza kuwa mvua za msimu zinatarajiwa kuanza kusambaa katika maeneo mengi nchini mwezi Novemba. Hata hivyo, baadhi ya maeneo ya Tabora, Katavi, Kigoma, Lindi na Mtwara yanatarajiwa kuanza kupata mvua hizo mapema, kuanzia wiki ya nne ya Oktoba hadi wiki ya kwanza ya Novemba.

Aidha, mvua hizo zinatarajiwa kuisha katika maeneo mengi nchini kati ya wiki ya tatu na ya nne ya Aprili 2027. Hata hivyo, baadhi ya maeneo ya magharibi na nyanda za juu kusini magharibi yanatarajiwa kuendelea kupata mvua hadi wiki ya kwanza ya Mei.

Kutokana na utabiri huo, tahadhari imetolewa kuhusu uwezekano wa kutokea kwa mafuriko, milipuko ya magonjwa na uharibifu wa miundombinu. Hali hiyo inasisitiza umuhimu wa wananchi na mamlaka husika kujiandaa mapema na kuzingatia taarifa pamoja na tahadhari zinazotolewa na mamlaka za kitaalamu.

Leave a Comment