
Omary Mkweva, mkazi wa Goba Kibururu jijini Dar es Salaam, anaomba msaada wa kifedha kutoka kwa Watanzania baada ya kukabiliwa na tatizo la kiafya linalomfanya ashindwe kutembea, kukaa na kupata haja kubwa na ndogo kwa takribani mwezi mmoja.
Omary anapitia kipindi kigumu kutokana na hali hiyo, ambayo pia imeambatana na kuvimba kwa sehemu ya tumbo lake, hasa eneo la kitovu, huku akieleza kuwa amepata pia uvimbe mkubwa kwenye shavu.
Kutokana na hali hiyo, Omary ameiomba jamii kumsaidia kifedha ili aweze kufika hospitalini kwa ajili ya uchunguzi wa kina na kupata matibabu kulingana na tatizo linalomkabili.
Hadi sasa, chanzo cha hali hiyo hakijawekwa wazi, hivyo uchunguzi wa kitabibu unahitajika ili kubaini tatizo na hatua zinazopaswa kuchukuliwa.
Kwa mujibu wa taarifa iliyosambazwa na Imelda Mtema, Omary anahitaji msaada wa watu wenye moyo wa kujitolea ili aweze kupata huduma za afya na kufanyiwa uchunguzi zaidi.
Kwa yeyote aliyeguswa na hali yake na mwenye uwezo wa kumsaidia, mchango unaweza kutumwa kupitia namba ya simu 0686891771, iliyosajiliwa kwa jina la Omary Mkweva.
Jamii inahimizwa kumsaidia kwa kadiri ya uwezo wake ili aweze kupata huduma za afya anazohitaji.
HABARI NA IMELDA MTEMA | GPL NA GLOBAL TV ONLINE