
Chama Cha Mapinduzi (CCM) kimesema ziara za Rais wa Zanzibar, Dkt. Hussein Ali Mwinyi, nje ya nchi zinalenga, pamoja na mambo mengine, kutafuta suluhisho la kudumu la changamoto ya umeme visiwani Zanzibar.
Aidha, ziara hizo zinalenga kuongeza tija katika uzalishaji wa ndani na kukuza matumizi ya nishati mbadala kwa ajili ya kuimarisha maendeleo ya Zanzibar.
Kauli hiyo imetolewa na Katibu wa Kamati Maalum ya Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya CCM Zanzibar, Idara ya Itikadi, Uenezi na Mafunzo, Khamis Mbeto Khamis, alipoulizwa kuhusu ziara za Rais Dkt. Mwinyi nje ya nchi.
Akijibu swali hilo, Mbeto alisema kuwa akiwa mjini Yeosu, Korea Kusini, Rais Dkt. Mwinyi amekutana na viongozi wa kampuni ya WongWang Electric Power Corporation (WG Corporation).
Alisema katika kikao hicho, pande hizo mbili zilijadili changamoto na fursa za ushirikiano katika uzalishaji, uhifadhi na usambazaji wa umeme.
Aidha, CCM imesisitiza kuwa itaendelea kuishauri Serikali kutumia fursa mpya za ushirikiano na kuendeleza misingi iliyowekwa na viongozi wa awamu zilizopita ili kuharakisha maendeleo ya nchi.
Mbeto alisema kampuni hiyo ya Korea Kusini iko tayari kutuma wataalamu wake Zanzibar kwa ajili ya kufanya tathmini ya mahitaji ya kiufundi na kubaini maeneo yanayoweza kutekelezwa miradi ya nishati.
“Katika ulimwengu unaokabiliwa na ushindani, Rais wa nchi hajifungii Ikulu. Badala yake, hutoka na kushiriki katika mawindo ya kiuchumi. Kama si yeye mwenyewe, basi wasaidizi wake hubeba majukumu hayo,” alisema Mbeto.
Akifafanua kuhusu hatua hiyo, alisema inalenga kuongeza uhakika wa upatikanaji wa umeme, kupunguza utegemezi wa nishati hiyo kutoka Tanzania Bara na kuweka msingi imara wa maendeleo endelevu Zanzibar.
“Akimaliza ziara yake huko Yeosu, Rais Dkt. Mwinyi ataelekea Kisiwa cha Jeju kushiriki Jukwaa la 27 la Sera za Utalii kwa Visiwa (ITOP Forum 2026). Jukwaa hilo litajadili utalii endelevu na kuimarisha ushirikiano wa maendeleo baina ya Zanzibar na Korea Kusini,” alieleza.
Mbeto pia alisema kuwa ushiriki katika majukwaa ya kimataifa, kikanda na yale yanayowakutanisha wataalamu ni muhimu katika kuimarisha ushirikiano na kuchochea maendeleo katika ulimwengu wa sasa.
“Kiongozi wa nchi hasafiri kwa ajili ya kutalii, bali kwa malengo mahususi ya kuipigania nchi yake na wananchi wake katika masuala ya maendeleo,” alisisitiza.
Aliongeza kuwa mabadiliko ya maendeleo yanayoendelea kuonekana Unguja na Pemba yanatokana na mikakati ya ushirikiano, ushiriki na ushirikishwaji katika fursa zinazopatikana duniani.
Mbeto alisema Rais Dkt. Mwinyi ataendelea kufanya ziara za nje ya nchi kwa lengo la kutafuta fursa za kiuchumi, kujifunza kutoka kwa mataifa mengine na kuimarisha nafasi ya Zanzibar katika jumuiya ya kimataifa.