Tukio la kuhuzunisha lililotokea Alhamisi iliyopita katika eneo la Crotona, Bronx, New York nchini Marekani la kijana mwenye asili ya Ghana, Javits Frimpong kupigwa risasi na kupoteza maisha wakati akielekea shuleni, limeamsha hasira kali kwa jamii ya watu na wanaharakati wa kupinga ubaguzi wa rangi, wakitaka haki itendeke.
Siku moja kabla ya kupigwa risasi, Javits alikuwa akitimiza mwaka mmoja tangu baba yake alipomchukua kutoka nchini Ghana, nyumbani kwao na kusafiri naye hadi Marekani ambako aliendelea na masomo.
Siku kadhaa baada ya tukio hilo, taarifa zinaeleza kuwa bado vijana waliotekeleza mauaji hayo, wanaotajwa kuwa ‘weupe’, bado hawajakamatwa, jambo linalozidi kuchochea hasira ya ubaguzi wa rangi.
Wakazi wa eneo la Bronx wamekusanyika kuomboleza kifo cha mwanafunzi huyo aliyeuawa kwa kupigwa risasi, wakilaani vikali tukio hilo. Viongozi wa dini, wanafamilia na wanajamii walikusanyika katika eneo ambalo kijana huyo alianguka baada ya kushambuliwa kwa risasi, kwa ajili ya kufanya ibada ya kumbukumbu na kumuombea marehemu.
Katika mkusanyiko huo, viongozi wa dini waliwaomba vijana kuacha vitendo vya vurugu vinavyoendelea kusababisha vifo vya watu katika jamii hiyo. Tukio hilo lilihudhuriwa pia na watu ambao familia zao zimewahi kukumbwa na matukio kama hayo.
Miongoni mwa waliohudhuria alikuwa Leandra Feliz, mama wa Junior Guzman, kijana aliyeuawa mwaka 2018 akiwa na umri wa miaka 15 katika tukio lililodaiwa kuwa la kumtambua mtu kimakosa.
Guzman alishambuliwa kwa mapanga na watu 14 waliodaiwa kuwa wanachama wa genge la Trinitarios, ambapo alijeruhiwa shingoni na baadaye kufariki katika Hospitali ya St. Barnabas.
Akizungumzia sababu ya kuhudhuria na ujumbe wake kwa familia ya Frimpong, Feliz alisema amefika kuonyesha mshikamano kwa familia hiyo kutokana na kupoteza mtoto mwingine mwenye umri wa miaka 15.