
Msanii wa muziki kutoka Tanzania, Nandy maarufu kama African Princess, ametangaza rasmi ujio wa album yake mpya inayokwenda kwa jina la 911, ambayo inatarajiwa kutoka Novemba 27, 2026.
Nandy ametoa tangazo hilo usiku wa kuamkia Novemba 2, 2026, katika hafla maalumu ya kutangaza ujio wa album hiyo jijini Dar es Salaam, iliyofanyika huku akiwapa mashabiki ladha ya kazi hiyo mpya kwa kutambulisha wimbo wake unaoitwa OYA, ambao ni miongoni mwa nyimbo zitakazokuwemo kwenye album hiyo.
Katika hafla hiyo, Nandy aliimba wimbo wa OYA kwa mara ya kwanza mbele ya mashabiki na wageni mbalimbali waliohudhuria. Miongoni mwa mastaa walioonekana wakifurahia na kucheza muziki huo ni Lulu Diva, Zaiylissa na Linah.

Akizungumzia album hiyo, Nandy amefichua kuwa imehusisha wasanii kutoka nchi sita ambazo ni Uingereza, Ghana, Nigeria, Uganda, Tanzania na Jamaica, hatua inayoifanya kazi hiyo kuwa na ladha ya kimataifa.
Amesema awali alikuwa na hofu ya kutoa nyimbo nyingi, jambo lililomfanya kutoa nyimbo mbili pekee kwa mwaka, lakini kutokana na ushawishi na ushauri wa watu mbalimbali waliomtaka kufanya kazi kubwa zaidi, aliamua kuingia studio na kuandaa album hiyo.
Kwa mujibu wa Nandy, maandalizi ya album ya 911 yamechukua takribani miaka miwili kukamilika. Ameeleza kuwa nyimbo zilizomo zimepitia mchakato wa kina wa kusikilizwa na watu mbalimbali, ambao walitoa maoni na mapendekezo kabla ya kufanya maamuzi ya mwisho kuhusu nyimbo zitakazojumuishwa.
Album hiyo itakuwa na zaidi ya nyimbo 10, huku msanii huyo akieleza kuwa amewekeza umakini mkubwa katika kuhakikisha kila wimbo unakidhi matarajio yake na kutoa ubora anaoutaka kwa mashabiki wake.
Aidha, Nandy amebainisha kuwa baada ya uzinduzi huo, kutakuwa na matukio maalumu ya Listening Party nchini Uingereza pamoja na nchi mbalimbali za Afrika Mashariki, yatakayowapa mashabiki nafasi ya kuisikiliza album hiyo na kufurahia muziki wake mpya.
Kwa ujio wa 911, Nandy anatarajia kupanua wigo wa muziki wake kimataifa na kuwafikia mashabiki wapya kupitia ushirikiano na wasanii kutoka mataifa mbalimbali.